Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Mhe. Juma Kilimba amewataka viongozi wa miradi mbalimbali mkoani hapo kuongeza juhudi katika usimamizi wa miradi wanayoitekeleza ili kulinda thamani ya fedha za Serikali zinazotumika kukamilisha miradi hiyo.
Akiongea leo tarehe 16/8/2021 wakati wa kuhitimisha ziara yake kwa wilaya ya Iramba katika ukumbi wa Halmashauri hiyo Mhe. Kilimba amewapongeza viongozi hao kwa hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi na kuwataka kushughulikia baadhi ya changamoto ndogo ndogo walizozibaini katika miradi sita waliyoitembelea.
Miradi iliyotembelewa na Mwenyekiti wa CCM mkoa ni ile inayohusiana na ukarabati na ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Tumaini, ujenzi wa darasa moja katika shule ya msingi Ulyang’ombe, ujenzi wa zahanati moja (OPD), Matengenezo ya barabara kutoka Shelui kupita Mtoa hadi Ndago, mradi mwingine ni ule wa umeme wa ujazilizi katika vitongoji vya Pangani na Kintende pamoja na mradi wa miche ya miti katika eneo la Lulumba.
“Ujenzi wa Hospitali kata ya Mkunda iliyogharimu shilingi milioni 50, umaliziaji wa chumba cha darasa katika shule ya msingi Ulyango’ombe, ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 30.74 inayogharimu kiasi cha milioni 199.9, mradi wa umeme na ujenzi wa mabweni katika shule ya sekondari Tumaini na mradi wa huduma za misitu ni miradi ambayo imekuwa na faida kubwa kwa wananchi wa Iramba, tuhakikishe inakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyotarajiwa na Serikali.” Alisema Juma Kilimba
Amewataka viongozi wanaosimamia miradi hiyo kuongeza umakinifu katika usimamizi wa miradi pamoja matumizi sahihi ya fedha za Serikali ili kufikia lengo la kuwasogezea huduma wananchi kwa ukaribu.
Aidha, Mhe, Juma amewapongeza wanachi wa wilaya ya Iramba kwa kujitokeza kwa hali na mali katika kuchangia ujenzi wa hospitali na shule mbalimbali wilayani hapo na kuwataka wananchi wa wilaya za jirani kuiga ushiriki wa shughuli za maendeleo badala ya kuiachia Serikali .
Mkandarasi wa kampuni ya M/S chase investment group ltd ya mkoani Mwanza inayosimamia ujenzi wa barabara hiyo, amesema ujenzi umegharimu kiasi cha shilingi 199,917,000 ikihusisha kuchonga barabara km 30,74 Kuweka changarawe km 13, ukarabati wa makalavati saba (7) na ujenzi wa makalavati mapya mawili (2) pamoja na kuchimba mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa mita 2694.5.
Ziara hiyo wilayani Iramba imewahusisha baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa, RC ambaye aliwakilishwa na DC Mhe. Paskasi Muragili pamoja na DC wa Iramba Mhe. Suleimani Mwenda na wakuu wa Idara mbalimbali.
MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA
Mradi wa ujenzi wa mabweni katika shule ya sekondari Tumaini
Mradi wa miche ya miti katika eneo la Lulumba
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.