MKOA wa Singida umezindua kampeni ya awamu ya tatu ya chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa polio ambapo watoto 363,315 wenye umri chini ya miaka mitano wanatarajia kupewa chanjo hiyo ili kujikinga na maradhi hayo.
Uzinduzi wa kampeni hiyo ya utoaji wa chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa polio kimkoa uliofanyika leo (Septemba Mosi, 2022) katika Halamshauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani hapa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro, alisema hayo leo katika alisema chanjo hiyo imeanza kutolewa leo Septemba Mosi itaendelea hadi 4 Septemba 2022.
Alisema ili kuhakikisha malengo ya kuwafikia watoto hao yanatimia, kila halmashauri ya mkoa huu ihakikisha inawafikia walengwa wake wa chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa Polio.
Alitoa mchanganuo kuwa katika chanjo hiyo, wilaya ya Iramba inatarajiwa kuwafikia watoto 56,360 ,Wilaya ya Singida vijijini watoto 58,197, Manyoni 45,416 Manispaa ya Singida watoto 39,841, Wilaya ya Ikungi 77,638, Wilaya ya Mkalama watoto 51,658 na Itigi watoto 34,205.
Alisema kauli mbiu ya kampeni hiyo ni "Kila tone la chanjo ya Polio litawekwa Tanzania salama dhidi ya Ugonjwa wa kupooza" ambapo kupitia kampeni hiyo inategemewa watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano watapatiwa chanjo.
Serukalmba alisema kuanza kutolewa kwa chanjo hiyo kunafuatia Shirika la Afya Duniani (WHO) ilipofika 17 Februari 2022 lilitoa taarifa ya uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa Polio (Wild polio Virus) nchini Malawi ambapo hadi sasa Malawi imeripoti visa viwili toka mlipuko huu utangazwe mwezi huo.
Aidha, nchi ya Msumbiji imeripoti visa vinne (4) ambapo kisa cha kwanza nchini humo kiliripotiwa mwezi Mei, 2022.
Alisema kufuatia kuonekana kwa ugonjwa huo wa Polio katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika, WHO ilitoa tamko kuwa Ugonjwa wa Polio ni janga la Kimataifa (Public Health Emergence of International Concern).
Mkuu huyo wa mkoa alisema tamko hilo la WHO lilikuwa na maana kuwa kugundulika kwa mtoto mmoja mwenye ugonjwa huu kuna uwezekano wa uwepo wa watoto zaidi ya mia mbili wenye maambukizi na uwezo wa kuambukiza watoto wengine na hata watu wazima ambao hawajapata chanjo.
"Shirika la Afya Duniani (WHO) linaelekeza kuwa unapotokea mlipuko au tishio la mlipuko wa ugonjwa wa Polio nchini, nchi husika na nchi jirani zinapaswa kufanya Kampeni ya kutoa chanjo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano (5) kwa awamu nne mfululizo ili kila mtoto aweze kupata kinga kamili," alieema Serukamba.
Aliongeza kuwa kufuatia mlipuko wa ugonjwa huu katika nchi za Malawi na Msumbiji, na kwa kuzingatia ukaribu wa kijiografia na mwingiliano wa watu kati ya Tanzania, Malawi na Msumbiji kwa shughuli za kiuchumi na kijamii, kuna uwezekano mkubwa wa maambukizi ya Ugonjwa wa Polio kusambaa na kuingia nchini.
Serukamba alisema ili kuweza kudhibiti ugonjwa huu usiingie nchini na kwa kuzingatia Mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wadau wa huduma za chanjo nchini inatekeleza Kampeni ya kutoa Chanjo ya Polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
"Awamu ya kwanza ya kampeni ilifanyika 24 hadi 27 Machi 2022 na ilitekelezwa katika mikoa minne inayopakana jirani na nchi ya Malawi ambayo ni Mbeya, Songwe, Njombe na Ruvuma. Kampeni hii ililenga kuwafikia watoto 975,839 wenye umri chini ya miaka mitano, na kufanikiwa kuwafikia watoto 1,130,261 sawa na asilimia 115 ya walengwa wote," alisema Serukamba.
Alisema katika awamu ya pili ya Kampeni hii ilifanyika nchi nzima kuanzia tarehe 18 hadi 21 Mei, 2022 ikilenga kuwafikia Watoto 290, 485 wenye umri chini ya miaka mitano, na kufanikiwa kuwafikia watoto 363,315 sawa na asilimia 125 ya walengwa wote ndani ya Mkoa wa Singida.
"Mkoa wa Singida unawapongeza na kuwashukuru Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wataalamu wa Afya, Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa, Vyombo vya Habari na wananchi kwa kufanikisha vyema utekelezaji wa Kampeni hii kwa awamu ya kwanza na ya pili," alisema Serukamba.
MWISHO
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.