Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amesema taasisi za dini ni nguzo muhimu katika kujenga maadili, kuimarisha umoja wa kitaifa na kukuza utii wa sheria miongoni mwa wananchi, akisisitiza kuwa maendeleo ya taifa yanahitaji jamii yenye hofu ya Mungu.
Dkt. Mganga alitoa kauli hiyo alipokuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangia ununuzi wa vyombo vya muziki vya Kanisa la EAGT Nduguti, Wilaya ya Mkalama, yenye lengo la kukusanya Shilingi milioni 15. Alieleza kuwa vyombo hivyo vitatumika kuimarisha ibada, mafundisho ya kiroho na semina zitakazochangia mabadiliko chanya ya kijamii.
Alifafanua kuwa hofu ya Mungu hujengwa kupitia malezi na mafundisho yanayotolewa na taasisi za dini, hali inayosaidia kupata raia watiifu, wanaozingatia sheria na kuepuka vitendo vya rushwa, ufisadi na uhalifu. Alisisitiza kuwa jamii yenye misingi imara ya kiroho ni msingi wa utawala bora na amani ya kudumu.

Aidha, Dkt. Mganga alisema shughuli hiyo imeonesha mshikamano wa kijamii kwa kuwakutanisha wananchi wa imani tofauti kushiriki lengo moja la maendeleo. Alieleza kuwa ushiriki wa viongozi wa Serikali, viongozi wa dini na wananchi kwa pamoja unaimarisha umoja na ushirikiano unaohitajika katika kujenga taifa lenye maadili.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkalama, Bi. Happyness Sulle, alisema taasisi za dini zimekuwa washirika wakuu wa Serikali katika kuhubiri amani, maadili na mshikamano, hususan kwa vijana, jambo linalochangia utulivu na maendeleo ya wilaya hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Bi. Asia Messos, alisema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo, akibainisha kuwa maendeleo ya jamii yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na taasisi za dini.
Akizungumza kwa niaba ya Kanisa la EAGT Nduguti, Mchungaji wa Kanisa hilo alisema taasisi za dini zitaendelea kuwa mstari wa mbele katika kukuza maadili mema, kupunguza vitendo vya uhalifu na kuijenga jamii yenye hofu ya Mungu kwa kushirikiana na Serikali.
Harambee hiyo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ibada, malezi ya kiroho na mshikamano wa kijamii, kwa lengo la kujenga taifa lenye maadili, umoja na utii wa sheria.








https://www.youtube.com/watch?v=M7aatIDpxbI&pp=ygUJU2luZ2lkYXJz
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.