Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe Halima Dendego,ametoa wito kwa taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali kutoa mafunzo kwa wanachama wa klabu za waandishi wa Habari katika Mikoa ili kuimarisha weledi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji na usambazaji wa Habari kwa umma.
Mhe. Dendego ameyasema hayo leo Januari 28,2025 wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wanachama wa klabu za waandishi wa habari wa mikoa ya Dodoma na Singida kuhusu matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 na tafiti nyingine za Takwimu yaliyoandaliwa na Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
“Kufanya hivyo kutaongeza kutangazwa kwa shughuli nyingi zaidi za maendeleo zinazofanyika mikoani zikiwemo zinazofanywa na wananchi wenyewe kama kilimo, ufugaji, uvuvi na nyinginezo nyingi ambazo zinagusa maisha ya siku ya wananchi sio tu wa vijijini bali hata wanaoishi mijini,”amesema Mhe.Dendego
Mhe. Dendego amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na Mpango Kabambe wa Pili wa Maendeleo ya Takwimu nchini (TSMP II).
Aidha ameseema kuwa Mafunzo hayo yanakwenda sambamba lengo kuu la Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Mwaka 2022 ambalo ni kuongeza uelewa, uwazi na kupanua wigo wa matumizi ya Matokeo ya Sensa kwa Serikali, wananchi na wadau wote ili kupanga mipango jumuishi kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na mazingira.
“Kamati za Sensa hazikuwa na uwezo wa kufika kila mahala lakini vyombo vya Habari vilifikisha ujumbe kila mahala bila kuwaacha wengine nyuma. Hivyo, sina budi kuvipongeza vyombo vyote vya Habari katika mikoa yetu ya Dodoma na Singida zikiwemo redio zetu za jamii kwa kujitoa kuelimisha na kuhamasisha wananchi kushiriki Sensa hadi tukafanikiwa kwa wananchi wote kuhesabiwa katika mikoa yetu” amesema Mhe Dendego
Hata hivyo amefafanua kuwa Lengo la Serikali ni kuona matokeo ya Sensa na ya tafiti nyingine za kitakwimu yanawafikia wadau wote hususani wananchi ili waweze kuyatumia katika shughuli zao binafsi na pia kuzitumia katika kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi ikiwemo kushiriki katika kufanya maamuzi ikiwemo kupanga, kufuatilia na kutathmini shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali na wadau wengine wa maendeleo katika maeneo yao wanayoishi.
Kwa upande wake Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Tanzania Bara Mhe Anne Makinda, amesema kuwa kwa sasa serikali ipo katika Awamu ya Tatu na ya mwisho ya utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi. Awamu hiyo inajumuisha uchakataji, uchambuzi na uandishi wa ripoti pamoja na usambazaji, kufanya mafunzo na kuhamasisha matumizi ya matokeo ya Sensa.
Ameeleza kuwa awamu hiyo ni tofauti na tafiti nyingine za kitakwimu ambazo matokeo yake hutolewa mara moja kwa mkupuo, matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi hutolewa hatua kwa hatua kufuatana na Kalenda ya Utoaji wa Matokeo. Kama mlivyoona wakati wa zoezi la kuhesabu watu, Dodoso la Sensa lilikuwa na maswali karibu ya 100, hivyo taarifa zilizokusanywa zilikuwa nyingi kwa maana hiyo uchambuzi wake hufanyika hatua kwa hatua hadi kupata matokeo na kutoa ripoti kamili. Matokeo ya Ripoti hizi yakishazinduliwa rasmi husambazwa kwa njia mbalimbali ili kuwafikia wadau.
Aidha amesema kuwa Mafunzo hayo kwa waandishi wa habari ni mfufulizo wa mafunzo yanayoendeshwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) ambayo yanafanyika kwa mujibu wa Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Mwaka 2022 na Lengo lake kuu ni kuvijengea uwezo waandishi katika kuchambua, kutafsiri na kutumia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na matokeo ya tafiti nyingine za kitakwimu zinazofanyika nchini ili viweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi zaidi.
Amesema mafunzo hayo yanaakisi msemo wa wahenga wa kupiga ndege wawili kwa jiwe moja. Kwa maana ya kutekeleza Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa na Mpango Kabambe wa Pili wa Maendeleo ya Takwimu nchini.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.