Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania-KKKT, Dk. Frederick Shoo, amesema uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ni mpango wa Mungu kuithibitishia Dunia kwamba wanawake wanao uwezo wa kuongoza nchi, kuliko hata wanaume.
Dk. Shoo ameyasema hayo Jumapili Oktoba 27, 2024, wakati wa ibada maalumu ya kuaga watumishi mbalimbali wastaafu, wakiwemo maaskofu, makatibu wakuu, watunza fedha na wasaidizi wao, waliowahi kulitumikia Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, tangu wakati wa Sinodi, mwanzoni mwa miaka ya 1960, hadi wakati huu wa KKKT, Dayosisi ya Kati.
"Ndugu zangu ni dhambi kubwa, kudharau mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii, kwa maendeleo ya Kanisa, hivi sasa kuna mfumo dume ambao umejengwa kwamba wanawake hawawezi, na mfumo huu haupo tu kwa jamii na kwenye siasa, bali upo hata kanisani kuwa wanawake hawawezi, leo nasimama hapa kuzungumza kwa niaba ya wanawake hawa, tuuone mchango wao, na tuwe wa wazo kwamba wanawake wanaweza," amesisitiza Dk. Shoo.
Hivyo, kutokana na hali hiyo, mtaalamu huyo wa masuala ya imani, hasa dini ya Kikristo, ameitaka jamii na Kanisa kwa ujumla, kuzidi kuwaunga mkono wanawake kwenye uongozi, Ili waweze kusimamia maendeleo yanayokusudiwa na jamii husika, pamoja na Serikali yao.
Kuhusu watumishi wanaoagwa, waliolitumikia Kanisa hilo kwa muda mrefu, Dk. Shoo amepongeza Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kati, kwa kuliona suala hilo jema, na akatoa rai kwa madhehebu mengine nchini, kuiga mfano huo, Ili kujenga heshima kwa wazee na familia zao.
Aidha juu ya uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa na ule mkuu wa mwakani (2025) Dk. Shoo amewataka Watanzania kijitokeza kushiriki zoezi hilo, na kuwachagua wanawake, pia na wanaume lakini wanyenyekevu, ambao jamii inawaona wana hofu ya Mungu, katika utumishi wao wa kuwaletea maendeleo.
Mkuu wa mkoa wa Singida, Halima Dendego, amesema ibada hiyo ni uthibitisho kwamba Kanisa hilo, linawathamini wazee hao, ambao walitumia muda wao mrefu wa maisha, kulitumikia Kanisa, ambalo hivi sasa linaonekana kupiga hatua kubwa ya maendeleo, katika nyanja mbalimbali.
Aidha Dendego amewaomba wageni waalikwa hasa familia za wastaafu waliokuja kutoka ndani na nje ya mkoa na nchi, waje wawekeze miradi mbalimbali, kutokana na hivi sasa mkoa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji, ikiwemo utalii, biashara, uvuvi, usafiri na utalii, na sasa Singida inakusudia kuwa Kituo kikuu cha cha kuliunganisha Taifa na kimataifa, kulingana na jiografia yake ya asili ilivyo.
"Kwa hiyo niseme sisi Singida, tunasema karibuni sana, lakini pia nina ombi langu hapa leo, tuna uchaguzi hivi karibuni, niwaombe sana ndugu wananchi, wale wote ambao wamejitathimini na wameona wanazo sifa, basi wasisite kugombea na sisi ndugu zao tutawachagua...kuhusu salamu za Rais tumeona hapa zilitolewa Dk. Syprian Hilinti asubuhi, tunayo imani kubwa sana na mama yetu mpendwa anayetuletea maendeleo," alisema Dendego.
MATUKIO KATIKA PICHA
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.