MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amewataka Makarani na Wasimamizi wa SENSA mkoani hapa wasifanye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kama ni la kuja kutafuta posho tu.
Akizungumza na Makarani na Wasimamizi hao ambao wanaendelea na mafunzo mjini Singida, alisema jukumu walilopewa ni kubwa sana linahitajika kufanywa kwa umakini ili taifa lipate takwimu sahihi za watu kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo.
"Zoezi hili ni kubwa la kitaifa ambalo linahitaji umakini wa hali ya juu na watakalofanya lifanikiwe ni nyie hivyo tusilifanye zoezi la Sensa kama ni la kuja kutafuta posho, inawezekana wengine wapo hapa na vishikwambi anayofundishwa haelewi kikubwa muhimu kwake apate hela jioni, utakuwa hujaisaidia nchi yako," alisema.
Serukamba alisema kupitia Sensa hii nchi itaweza kujua idadi ya maskini, watu wanahitaji shule, afya na maji kiasi gani hivyo vijana watambue wameaminiwa na nchi waifanye kazi ya Sensa kwa umakini sana.
Alisema mtihani kwa wasimamizi na makarani wa Sensa ni kuifanya kazi kwa weledi na kuleta takwimu sahihi ambapo wakiifanya vizuri kazi hii Serikali itakapokuwa na kazi nyingine wao ndo watapewa kipaumbele kupewa.
"Mkoa unawategemea sana kupata takwimu sahihi na kuufanya uwe miongoni mwa mikoa itakayofanya vizuri katika zoezi hili la Sensa ambalo hufanyika kila baada ya miaka 10," alisema.
Serukamba alisema makarani na wasimamizi watapewa madodoso hivyo ni muhimu wajifunze mbinu za kuwauliza wananchi ili kuwafanya wawaelewe watakapokuwa wakiwadadisi.
"Kuja mtu unaweza kumuuliza una ng'ombe wangapi akashindwa kueleza pengine akidhani unataka kuja kunyang'anya ng'ombe wao ...hapana ni muhimu kujifunza mbinu za kumfanya mtu akuelewe sababu majibu yenyewe yanatokana na maswali rahisi atakayoulizwa," alisema.
Aliongeza kwa mfano Tanzania inaelezwa ni nchi ya pili katika Afrika kwa kuwa na mifugo mingi baada ya Ethiopia lakini ukiuliza tuna ng'ombe au mbuzi wangapi hakuna anayejua.
Alisema Sensa inakwenda kuleta majawabu yote hayo kinachohitajika ni umakini kwa makarani na wasimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi walioaminiwa na Serikali kuifanya kazi hiyo kwa umakini na weledi wa hali ya juu.
Naye Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi Mkoa wa Singida, Mratibu wa Sensa Mkoa wa Singida, Naing’oya Kipuyo, makarani 445 wamehitimu mafunzo yao ya dodoso la Sensa ambalo watahoji majengo na makundi maalum.
Alisema kundi la pili ni la wasimamizi wa maudhui ambao watahoji dodoso la jamii ambao wapo 212 ambao wataendelea na mafunzo kwa siku tatu.
MWISHO
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.