MKUU wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi ametoa miezi miwili kwa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika wa mkoani hapa kuhakikisha anafanya ukaguzi kwa vyama vyote ambavyo bado havijakaguliwa, na kinyume chake hataruhusu mchakato wowote wa mikopo kufanyika.
Dkt. Nchimbi aliyasema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 3 wa Chama Kikuu cha Ushirika (SIFACU) mkoani hapa Oktoba 30, 2019.
“Ukaguzi kwenye vyama hivi ni lazima na sio hiari, nakuagiza mrajisi ndani ya miezi miwili vyama vyote vilivyobaki viwe vimekaguliwa na chama kisichokaguliwa kisipewe mkopo wowote,” alisema Nchimbi
Alisema kwa mkoa wa Singida inasikitisha kuona takwimu zinaonyesha kati ya jumla ya vyama 320 vilivyopo ni vyama 70 pekee ndivyo vilivyokaguliwa jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali chanya wa uhai wa ushirika na wanaushirika wenyewe.
Alisisitiza kuwa, ushirika pamoja na mambo mengine ni lazima daima utembee na ajenda ya mshikamano, nguvu, heshima na uhai endelevu, na kuweka kando masuala yote yanayoweza kuufifisha yakiwemo ubinafsi na migogoro isiyokoma.
“Utakuta kila siku vitu vinavyoleta utapiamlo kwenye vyama hivi vya ushirika ni ubinafsi…watu wamesahau kabisa kuwa ushirika ni utumishi ndio maana rushwa imetamalaki na matokeo yake ni kufifisha matarajio chanya,” alisema Nchimbi.
Akizungumza kwa msisitizo, Dkt. Nchimbi alisema anatamani moja ya ajenda kubwa ya wanaushirika wote iwe ni kutafuta suluhisho la lishe bora kwa watoto waliopo mashuleni ili hatimaye kuwawezesha kujenga utulivu wa akili kuweza kumsikiliza vizuri mwalimu na kumudu masomo yao.
Aidha, aliwakumbusha wanaushirika wote nchini, hususani wale wa mkoa wa Singida kutambua kwamba wao ni nguzo na mkono wa Serikali katika kushauri, kuongoza, kuelekeza na kuifikisha jamii na taifa kwenye uchumi wa viwanda kama ishara na tunda la Serikali ya Awamu ya TANO iliyopo madarakani kwa sasa.
Hata hivyo Dkt. Nchimbi alitumia fursa hiyo kuwasisitiza Wananchi hao waliojitokea katika kikao hicho kushiriki vyema katika zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura linaloendelea kutolewa mkoani Singida.
Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoani hapa, Bw. Thomas Nyamba, alisema hali ya vyama vya ushirika ndani ya mkoa wa Singida inaendelea kuimarika ikilinganishwa na huko nyuma, huku idadi ya vyama hivyo ikifikia 320.
“Tuna jumla ya vyama vya ushirika mia tatu na ishirini, kati ya hivyo sitini na tisa ni vile vya mazao hususani pamba na alizeti, huku upande wa saccos hali sio ya kuridhisha kutokana na vingi kati yake kukabiliwa na madeni,” alisema Nyamba.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa SIFACU, Bw. Yahaya Ramadhan Khamis alibainisha pamoja na mambo mengine lengo la mkutano huo mkuu ni kutathmini shughuli zote zilizofanywa kwa mwaka uliopita na kupanga mipango ya mwaka unaoanza.
“Mwaka uliopita tumefaulu kuunganisha vyama na wanachama wake kutoka idadi ya vyama thelathini na sita hadi sitini na sita, tumeweza pia kutafuta masoko ya uhakika, kuwaunganisha wakulima kuweza kupata mikopo kwenye taasisi za fedha,” alisema Khamis
Shamrashamra za ufunguzi zikiendelea
Waddau mbalimbali wakiwa na Wanachama wa Ushirika wa mkoani
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoa wa Singida Bw. Khamis Rajab Mwanjowa akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa 3 wa Chama Kikuu cha Ushirika (SIFACU) mkoa wa Singida Oktoba 30, 2019.
Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Singida Bw. Thomas Nyamba akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa 3 wa Chama Kikuu cha Ushirika (SIFACU) mkoa wa Singida Oktoba 30, 2019.
Mkutano ukiendelea
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akisisitiza washiriki wa Mkutano huo kushiriki kikamilifu katika zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura.
Picha za pamoja
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi wakati wa kukagua mabanda ya Wajasiriamali
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.