Mkuu wa mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego ameahidi kushughulikia kwa haraka mkwamo wa ujenzi wa majengo Matatu (3) katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida iliyopo Kata ya Mandewa katika Manispaa ya Singida, jengo la ghorofa Tatu linalotarajiwa kutoa huduma za kibingwa ikiwemo upasuaji wa mifupa, wodi za watoto, huduma za wagonjwa mahutututi, maabara na huduma za ufamasia.
Jengo hilo la ghorofa Tatu ujenzi wake ulianza mwaka 2014 na kusimama kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo Mkandarasi aliyekuwa anajenga jengo hilo kusimamishwa kuendelea na ujenzi kutokana na uwezo mdogo katika utekelezaji wa mradi huo.
RC Dendego ametoa kauli hiyo katika kikao na Watumishi wa Hospitali hiyo cha kusikiliza kero na kukagua majengo ambayo ujenzi wake umesimama na kusisitiza kuwa atalibeba jambo hilo na kulifanyia kazi ili ujenzi huo uweze kuendeleo na kukamilika kwa haraka lengo likiwa ni kuongeza utoaji wa huduma za matibabu kwa wananchi karibu na maeneo yao.
“Mimi ni Muumini ya Namba Moja kwa kila jambo hivyo nataka Hospitali hii ya Rufaa ya Mkoa iweze kushika Namba 1 nchini na Dunia kwa ujumla kwa utoaji huduma za kiwango cha juu za afya kwa wananchi kwani Hospitali nyingine wanaweza kwa nini sisi tushindwe na Serikali imewezesha vifaa na Watumishi wapo” Amesisitiza RC. Halima Dendego.
Kuhusu Watumishi wanaojitolewa kwa muda mrefu bila kupata ajira, Mkuu huyo wa mkoa ameutaka Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kumpatia orodha ya Watumishi wote wanajitolewa lakini hawajapata ajira ili aweze kuwasaidia katika ngazi husika.
Hata hivyo, Mhe. Dendego amewapongeza Watumishi hao kwa kufanya kazi kwa bidii bila kukata tamaa kutokana na kutopatiwa ajira na kusisitiza kuwa jambo hilo atalishughulikia ili watumishi hao waweze kupata ajira za kudumu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida Martha Mlata, amewasisitiza Watumishi wa Hospitali mkoani humo kuendelea kuchapa kazi bila kuchoka kwa viwango vya juu kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita inawajali na itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa muda muafaka.
Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida Dkt. David Mwasota ameishukuru Serikali kwa kuwa bega kwa bega na Watumishi wa afya ikiwemo kuwapatia vitendea kazi vya kisasa na kuboresha maslahi yao hivyo jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi ili wasiende mikoa mingine kufuata huduma hizo za afya.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida Dkt. David Mwasota, akitoa taarifa ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida iliyopo Kata ya Mandewa Singida Mjini. Juni 3, 2024
Ukaguzi wa Majengo ukiendelea
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.