Wasimamizi wa Vikundi vya Vijana wajasiriamali wadogo wadogo mkoani Singida wametakiwa kuvishauri na kuvisaidia vikundi hivyo kwa kuangalia mipango kazi yao kabla ya kuwakopesha ili fedha watakazozipata waweze kuzitumia vizuri na kuwaletea maendeleo.
Maagizo hayo yametolewa Januari 20, 2022 na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Alhaji Juma Kilimba alipokuwa akikagua kikundi cha vijana kilichopo Iguguno katika wilaya ya Mkalama kinachofahamika kwa jina la Iguguno Youth Group ambacho kinajishughulisha na ufatuaji wa matofali na ufugaji wa kuku wa kienyeji.
Ziara hiyo ya kamati ya siasa imeingia siku ya pili ikiwa na lengo la kukagua miradi iliyojengwa kwa fedha za uviko 19, fedha zitokanazo na tozo za miamala ya simu pamoja na mapato mbalimbali ya Halmashauri.
Aidha Alhaji Kilimba amesema vikundi vyote vinavyokopeshwa fedha za Serikali ni lazima vilelewe vizuri ili vikomae na kufikia kikomo na kupisha vikundi vingine viweze kukua hivyo akawataka Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa na Wilaya kuhakikisha wanawashauri na kuwaongoza hasa katika kipidi wanapowakopesha fedha ili waweze kufikia malengo yao.
“Ni lazima elimu itolewe kwa wanakikundi wajue namna ya kuandika mahesabu ya mapato na matumizi wapate elimu juu ya namna ya kupambana na majanga yanayoweza kujitokeza katika biashara zao pamoja kuendeleza mitaji iweze kukua” alisema Bwana Kilimba.
Hata hivyo ameitaka Serikali kuvisaidia vikundi hivyo kupata masoko ya bidhaa wanazozalisha kama sehemu ya kuwaunga mkono hali itakayosaidia kushawishi vijana wengine kujiunga au kuanzisha vikundi mbalimbali vyenye kuongeza ajira na vipato kwa vijana.
Awali akisoma taarifa ya kikundi hicho Bi Winifrida Innocent katibu wa kikundi amesema Halmashauri ya Mkalama iliwakopesha fedha kiasi cha Sh. Milioni 15 ambazo zilitumika kununua baadhi ya vifaa kama mashine ya umeme na inayotumia mikono kwa ajili ya kufyatulia matofali, vibao pamoja na sement.
Aidha ameishukuru Halmashauri ya Mkalama kwa kuwa imekuwa ikiwasaidia ushauri na wataalamu ambao wamekuwa wakiwatembelea mara kwa mara.
Hata hivyo ziara hiyo ya Kamati ya siasa imefanyika katika wilaya mbili za Mkalama pamoja na Iramba ambapo walikagua miradi ya maji, madarasa na kituo cha afya ambapo kamati hiyo imeridhishwa na ujenzi ulivyofanyika na namna ambavyo watoto wamekuwa wakiendelea kusajiliwa katika mashule hayo.
Hata hivyo Mwenyekiti amesisitiza utunzaji wa miradi hiyo ili iweze kusaidia vizazi vijavyo hasa katika vyumba vya madarasa na thamani zake wakati kwenye miradi ya maji akiwataka wataalamu kuhakikisha maji yanasambazwa karibu na makazi ya watu.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.