Kamati zinazoshughulikia changamoto ya ugawaji wa mashamba ya korosho wilayani Manyoni zimepewa Siku Saba kuanza tarehe 25 April 2022 kugawa na kuwaonesha mashamba wakulima wa zao hilo lengo likiwa ni kuhakikisha ifikapo Octoba 2022 yawe yamekwisha safishwa na kilimo kimeanza.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge alipokutana na wakulima zaidi ya Mia na hamsini katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Manyoni waliokuwa wakilalamikia mchakato wa ugawaji wa mashamba kugubikwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kukosa mashamba kwa wakulima waliolipia, mashamba kutosafishwa wakati yalishalipiwa na bàadhi ya wakulima walilipa fedha kwa muda mrefu lakini hawajaoneshwa mashamba yao.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza wakati wa kikao hicho
RC Mahenge ameagiza kamati hizo kutumia Siku Saba kuanzia Siku ya tarehe 25 April kutambua majina ya wote wanaotakiwa kupatiwa mashamba na kuanza kuwaonesha mashamba yao huku akisisitiza kwamba hakuna mtu atakayepoteza haki yake.
Aidha ameagiza kuandaliwa andiko na mihtasari ya mikutano inayofanyika ili kusaidia usimamizi wa mashamba hayo na kurahisisha ufuatiliaji wakati wanapokuja viongozi wapya.
RC Mahenge amesema utaandaliwa utaratibu mzuri wa mawasiliano baina yao na wenye mashamba ili kuondoa changamoto hizo ambazo zimedumu kwa miaka zaidi mitatu.
"Changamoto zote zilizotokea mpaka kusababisha migogoro katika ugawaji wa mashamba na kutuchelewesha kwa miaka mitatu limesababishwa na ufuatiliaji na usimamizi mbaya uliofanywa na bàadhi ya Maafisa wa Serikali, lazima tutengeneze utaratibu mzuri utakaosaidia kuendeleza zao la korosho mkoani hapa" alibainisha Dk. Mahenge.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko akizungumza wakati wa kikao hicho.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko amesema wamedhamiria kuondoa changamoto zilizojitokeza na watahakikisha kwamba ifikapo Oktoba 2022 mashamba yote yatakuwa yamekamilika ili kuongeza uzalishaji wa Korosho na kuongeza mapato ya Wilaya hiyo na Mkoa kwa ujumla.
Hata hivyo RAS huyo amewataka wakulima kuiamini timu inayoshughulikia matatizo ya changamoto hizo na kutoa ushirikiano pale utakapohitajika ikiwemo ukaguzi wa nyaraka za malipo na mahitaji mengine.
Aidha kwa kuanza kubadisha utaratibu RAS akabadilisha Mratibu wa Awali na kumteua Bwana Lucas Mkuki Afisa kilimo kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuendeleza uratibu wa ugawaji wa mashamba ambapo atafanya kazi kwa kushirikiana na kamati zitakazokuwepo.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wengine Abdala Mbonde ameishukuru Serikali ya Mkoa kwa maamuzi yao ya kuhakikisha changamoto zinatatuliwa na kilimo cha korosho kinaanza.
Mbonde ameshauri kamati itakayoundwa ihakikishe haki inatendeka ili wakulima hao waweze kuendelea na uwekezaji huo katika kilimo hicho kwalengo la kujikwamua kiuchumi.
Mkutano ukiendelea
http://singidars.blogspot.com/2022/04/singida-kutatua-mgogoro-wa-mashamba-ya.html
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.