Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amewataka wananchi wa Mkoa wa Singida kuwekeza zaidi katika kilimo cha alizeti kutokana na fursa kubwa ya uzalishaji inayopatikana katika mkoa huo pamoja na udongo wake kuwa na rutuba inayofaa kwa zao hilo.

Akizungumza leo katika kijiji cha Mnang’ana, kata ya Sepuka, Wilaya ya Ikungi, Mhe. Dendego amesema alizeti ni zao la kimkakati kwa mkoa huo kwani linaweza kuwa chanzo kikubwa cha kipato kwa wakulima na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa.

Akijibu swali la mdau kuhusu mkakati wa mkoa katika kuhakikisha upatikanaji wa mazao bora ya alizeti, Mkuu wa Mkoa amesema kupitia sekta ya kilimo, mkoa umeandaa mbegu bora za alizeti chotara zenye ustahimilivu na uwezo wa kutoa mavuno makubwa.

“Tunawahimiza wakulima kuchangamkia fursa hii kwa kutumia mbegu bora tulizozitayarisha, kwani zitasaidia kuongeza uzalishaji, kipato na kuboresha maisha ya wananchi,” amesema Mhe. Dendego.
Kadhalika,Katika hotuba hiyo, Mhe. Dendego amesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kutoa malezi bora kwa watoto wao ili kukabiliana na changamoto ya mmomonyoko wa maadili unaoendelea kushuhudiwa katika jamii.
Amesema wazazi wanapaswa kuwafuatilia watoto wao kwa karibu, kuwalea kwa misingi ya maadili mema, na kuhakikisha wanapata malezi bora yanayojumuisha elimu ya darasani pamoja na malezi ya kiutu na kiutamaduni.

“Wazazi mna jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wetu wanakua katika maadili mema, wanaheshimu mila na tamaduni za Kitanzania, na kuwa raia wema wa kesho,” amesisitiza.
Hayo yalijiri wakati Mhe. Dendego aliposhiriki katika zoezi la upandaji wa miti lililoandaliwa na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Tanzania kupitia BAKWATA Mkoa wa Singida, ambapo alipanda mti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika eneo la Msikiti wa Mnang’ana pamoja na Shule ya Msingi Mnang’ana.

Katika zoezi hilo, viongozi wa dini walihimiza jamii kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda na kutunza miti, wakisisitiza kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya ibada na mchango muhimu katika kulinda uhai wa binadamu.






SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.