Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego, ameagiza kuchukuliwa hatua kwa Wakuu wa Idara ambao watazalisha hoja mpya za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kama hatua ya kuimarisha utendaji kazi kwenye Halmashauri hizo.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida ametoa kauli hiyo (26/Juni/2024) katika Kikao Maalum cha kujadili hoja za CAG cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
Dendego ametoa agizo hilo kufutia Halmashauri ya Manispaa ya Singida kuwa na hoja 64 kutoka mwaka wa fedha 2011 hadi Juni 2024 ambazo hazijafungwa jambo ambalo amesema sio zuri na linatia dosari katika kutekeleza sheria, kanuni na taratibu za Serikali hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ameonya kuwa hataki kusikia uzalishaji wa hoja mpya zinazalishwa tena na kama zikitokea basi aliyesababisha hoja hiyo aitwe na kuhojiwa kwa nini hoja hiyo imetokea ikiwezekana achukuliwe hatua kwa kusababisha hoja hiyo.
Amesema hoja hizo zinapotokea zinasababishwa na kuwepo kwa kasoro hasa katika usimamizi hafifu wa miradi ya maendeleo.
Naye, Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga ameonyesha kukerwa na uwajibikaji hafifu wa Watendaji wa Manispaa ya Singida katika kujibu hoja za CAG licha ya ushauri uliowapatia katika kikao cha Kamati ya Fedha.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu, amemhakikishia Mkuu wa mkoa wa Singida kuwa watafanyia kazi maelekezo yao ili kuhakikisha hoja 64 za CAG zinafanyiwa kazi ili kuhakikisha Manispaa ya Singida inakuwa bora katika utendaji wake wa kazi.
Dkt. Mganga amesema mambo mengi walioshauri ambayo yangesaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza hoja za CAG hayajafanyiwa kazi jambo ambalo ameonya lazima likome na Watendaji lazima wawajibike ipasavyo katika kuondoa kasoro hizo.
Amewataka Wakuu wa Idara katika Halmashauri za mkoa huo kuacha uzembe na kuhakikisha hawazalishi hoja mpya za CAG na kujibu kwa uhakika hoja zilizopo ili ziweze kufungwa na CAG.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.