Wamiliki wote wa migodi inayofanya shughuli za uchimbaji wa madini Mkoani Singida wameagizwa kuhakikisha kuwa hakuna vifo wa majeruhi katika maeneo yao kutokana na uwepo wa miundombinu mibovu au uzembe wowote.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ametoa agizo hilo alipotembelea mgodi wa madini katika Kijiji cha Konkilangi, Kata ya Ntwike, Tarafa ya Shelui, Wilaya ya Iramba kuona shughuli za uokoaji mara baada ya mgodi huo kutitia huku watu wawili wakihofiwa kufariki.
Dkt Nchimbi amesema wamiliki wa migodi wanatakiwa kuwekeza katika kuboreha miundombinu ya migodi ili wachimbaji waweze kufanya kazi katika mazingira ambayo si hatarishi.
“Madini yanatakiwa kuleta neema na kukuza uchumi wa taifa letu na sio kuangamiza nguvu kazi na kuleta majonzi, serikali haiwezi kukubali kupoteza vijana kutokana na uzembe wa baadhi ya watu”, amesema.
Ameongeza kwa kumtaka Kamishna Msaidizi wa madini kanda ya kati Sostenes Masolla kuweka ratiba ya kutoa mafunzo kila wiki huku akitakiwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili wachimbaji wapewe semina na mafunzo ya juu ya usalama wao wawapo migodini.
Dkt Nchimbi pia amemtaka Kamishna huyo wa madini kufuatilia taaluma na sifa zinazotumika kuchagua wakaguzi wa migodi maarufu kama ‘inspekta’ kwakuwa wao ndio hutakiwa kwa kiwango kikubwa kuhakikisha kuwa shimo au duara liko salama kabla ya kuruhusu uchimbaji kufanyika.
“Hawa ma inspekta hawa wasituulie vijana kutokana na uzembe wao, unakuta hajakagua vizuri halafu anaruhusu watu walipue baruti matokeo yake ndio kama haya, hawa wakiwa makini ajali za kwenye migodi zitapungua sana”, amesisitiza.
Aidha Dkt Nchimbi amewataka wachimbaji na wamiliki wa migodi kuachana na imani potofu kuwa endapo vifo vinatokea katika shimo la mgodi hapo panakuwa na madini mengi.
Amesema ikiwa atabaini kuwa imani hizo zinaendekezwa na kipa endapo patatokea tena kifo katika mgodi huo basi hatasita kufunga shughuli za uchimbaji katika mgodi huo.
Kwa upande wao wachimbaji wameeleza kuwa ajali hiyo imesababishwa na uzembe wa mgakuzi wa shimo hilo ambaye aliruhusu ulipuaji wa baruti wakati mazingira yakiwa hayaruhusu.
Wachimbaji hao wamemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa wamekosa amani kutokana na vifo hivyo ambavyo kwa kiwango kikubwa vimetokana na uzembe huku pia wakilalamikia utaratibu wa malipo yao.
Mmoja wa wachimbaji hao Abuu Amiri amesema ma inspekta hao wamekuwa wakijali maslahi binafsi badala ya kuangalia usalama wa wachimbaji watakaoingia katika shimo hilo.
Mgodi ujulikanao kwa jina la Sekenke 1 katika kitalu namba 1, ambapo maduara matano yanayomilikiwa na Marijan Ramadhani na Jakobo Ntobi, yalititia mnamo tarehe tisa Septemba na kusababisha vifo kwa wachimbaji wawili huku mmoja tayari mwili wake ukiwa umepatikana na majeruhi watano.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.