Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Sophia Mfaume Kizigo amewataka wananchi wa Wilaya ya Mkalama iliyopo mkoani Singida kutunza miradi waliyoianzisha ili iweze kuwaongezea tija na kipato kwao na taifa kwa ujumla.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Sophia Mfaume Kizigo (katikati) akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mkalama
Akiongea baada ya uzinduzi na uwekaji wa jiwe la msingi katika miradi mbalimbali iliyokaguliwa na Mwenge wa Uhuru leo Julai 21, 2021 katika Wilaya hiyo amewataka wananchi kuhakikisha miradi inatunzwa ili kufikia malengo yaliyotarajiwa.
Amesema, miradi Zaidi ya nane ikiwemo ujenzi wa visima vya maji katika maeneo tofauti, ujenzi wa barabara, programu za kupambana na madawa ya kulevya pamoja na matumizi ya mifumo mbalimbali ni moja ya miradi iliyozinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru 2021 wilayani hapo.
“kuzinduliwa na uwekaji wa mawe ya msingi kwa miradi yetu ni ishara ya usimamizi mzuri wa miradi, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha kwamba tunaitunza miradi yetu ili iweze kutuletea mafanikio” alisema Mhe. Sophia.
Pia amewataka wana Mkalama kuhakikisha wanapata lishe bora ili kuendelea kupunguza udumavu kwa watoto na kwa wakina mama wajawazito.
Kiongozi maalum wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Lt. Josephine Paul Mwambashi (kushoto) akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Jorma wilayani Mkalama wakati wa uzinduzi wa Klabu ya kupinga rushwa.
Kwa upande wake Kiongozi maalum wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Lt. Josephine Paul Mwambashi ametoa wito kwa wanamkalama kuongeza ujuzi katika matumizi ya TEHAMA kwa kuwa huko ndipo ajira zinapopatikana.
LT. Mwambashi amebainisha kwamba masoko ya mazao na malipo mbalimbali ya huduma zinazotolewa na Serikali pamoja na mashirika mbalimbali yanapatikana katika mifumo ya TEHAMA.
Aidha LT. Mwambashi amebainisha kwamba matumizi sahihi ya mifumo mbalimbali ya kieletroniki yameonesha kusaidia nyanja ya usafirishaji, Afya pamoja na upatikanaji wa taarifa kwa wakati hivyo kuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya uchumi nchini.
Hata hivyo kiongozi huyo wa Mwenge kitaifa amewataka vijana kuepuka ngono zembe pamoja na utumiaji wa madawa ya kulevya ambayo kwa kiasi kikubwa vimekuwa vikikatisha ndoto za vijana wengi nchini.
Amesema mbio za Mwenge mwaka huu zitumike kupambana na magonjwa mbalimbali yakiwemo malaria na VVU/UKIMWI.
“Tufanye usafi wa mazingira pamoja na kufukia madimbwi ili kupambana na mazalia ya mbu wanaosababisha malaria, lakini pia tuhakikishe tunaepuka ngono zembe ili kuepuka ugonjwa wa VVU/UKIMWI” Alisema LT. Mwambashi
Hata hivyo amewakumbusha wananchi wa Mkalama kutumia vyandarua vyenye viuatilifu lengo likiwa ni kuhakikisha malaria inakwisha. Alisisitiza Lt. Josephine Paul Mwambashi.
Mratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mkoa wa Singida Fredrick Ndahani (kulia) akizungumza na wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa 2021 kuhusu lishe bora.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.