Timu ya usimamizi na uendeshaji wa huduma za afya Mkoa na Wilaya imeazimia kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wanajamii wote kwa usawa ikiwa ni pamoja na kushirikisha wanaume kikamilifu ili kuboresha afya zao wenyewe, afya za wanawake, watoto na vijana.
Hayo yamesemwa leo tarehe 12 Disemba, 2024 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwenye warsha yenye lengo la kuimarisha huduma za afya kwa kushirikisha wanaume katika huduma za afya ya uzazi, mama na watoto.
Bi-Desteria Nanyanga Mwakikishi kutoka Wizara ya Afya akitoa mafunzo amesema kuwa warsha hii ni muhimu kwani wanaume ndio watoa maamuzi katika familia na hii itasaidia kuvunja vikwazo vya kitamaduni, kuboresha huduma za afya ya uzazi kwa vijana, kupunguza ukatili wa kijinsia na kuhakikisha kuwa wanawake na watoto wanapata msaada muhimu wakati wa ujauzito, kujifungua, na baada ya kujifungua.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Bi Teda David Sinde akifungua warsha hiyo amesema matarajio yake mara baada ya warsha hiyo ni uelewa wa pamoja kuhusu ushiriki wa wanaume katika afya ya uzazi, mama na mtoto, kuboresha huduma za afya katika wilaya ya Ikungi na kutumia vyema uzoefu wao kutoa maoni ili mpango huu uweze kufanikiwa.
"Tunakusudia kuwasilisha na kukusanya maoni na mapendekezo ili kuboresha mwongozo huu na kuhakikisha unafaa kwa utekelezaji ngazi ya mkoa, Halmashauri na Jamii kwa ujumla" amesema
Kwa upande wake Bi-Nkinda Shekalagwe mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), amewaomba wote waliopata elimu hiyo kwenda kuwa walimu wazuri kwa wenzao ili kuhakikisha huduma za afya wilaya ya Ikungi zinakuwa vizuri katika upande wa Afya ya uzazi na lishe.
Wakitoa maoni yao katika warsha hiyo,baadhi ya wajumbe wamesema changamoto imekuwa ni umbali na uchache wa vituo vya kutolea huduma za afya, Mila na tamaduni za baadhi ya makabila juu ya mwanamke na mwanaume kuongozana kwenda vituo vya afya,hivyo wameomba elimu kutolewa zaidi kwa jamii ili kufuta dhana mbalimbali potofu zilizopo ili kuboresha huduma za afya.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.