WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaagiza Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia Watumishi wote katika Halmashauri za Mkoa wa Singida ambao walikusanya fedha za mapato lakini hawakuzipeleka benki wanazirudisha haraka.
Ametoa agizo hilo leo kwenye kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku mbili mkoani hapa wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri za Wilaya ya Singida, Ikungi na Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
Alisema kumekuwa na tatizo kubwa kwenye Halmashauri nyingi nchini katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo baadhi ya Watumishi wanapokusanya fedha haziingizwi kwenye mfumo wa Serikali jambo ambalo limekuwa kero kubwa.
"Wakuu wa Wilaya hakikisheni Watumishi wanaodaiwa fedha wazirudishe haraka, Iramba, Manyoni na hata Ilongero (Halmashauri ya Wilaya ya Singida) nimepewa orodha ya Watumishi ambao wanadaiwa fedha za makusanyo," alisema.
Majaliwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza suala la ukusanyaji wa mapato na hata majuzi wakati anawaapisha wakuu wa mikoa lakini cha kushangaza baadhi ya Watumishi wa umma wamegeuka kuwa wabadhirifu.
Alisema ujanja unaofanywa na baadhi ya Watumishi kufuja fedha za makusanyo ni kwamba wanapokusanya fedha hasa wanapobaini ni nyingi wanazima mashine ili zisiingie kwenye mfumo wa Serikali.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka Watumishi kuacha urasimu katika utendaji wa kazi kwani mambo hayo ndio yanakaribisha vitendo vya rushwa chini.
Kuhusu idara za manunuzi, alisema limekuwa ni tatizo kubwa ambapo Idara hizo zimekuwa zikiweka makadirio makubwa ya bei za manunuzi ya vifaa vya ujenzi kwenye miradi hususani inayotumia 'force account'.
Aliongeza kuwa kwenye Halmashauri kumekuwa na tatizo kubwa la usimamizi wa miradi inayotekelezwa na kwamba kuna umuhimu kwa Watumishi kuhakikisha suala hili linapewa umuhimu wa juu.
Alisisitiza suala la mahusiano kwa Watumishi wa Umma mahali pa kazi kwani kufanya hivyo kutaboresha utendaji kazi na kuleta ufanisi mkubwa katika kuwatumikia wananchi.
Aidha, alizitaka Halmashauri kuratibu vizuri suala la wafanyabiashara wadogo maarufu wamachinga ili wapewe maeneo ya kufanyia biashara zao bila usumbufu.
Waziri Mkuu (kushoto) akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida
Awali Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida linalojengwa Ilongero katika kijiji cha Mwahango kwa thamani ya Sh. 2.7 bilioni.
Akizungumza na wananchi wa eneo hilo, alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Ester Chaula, kuisimamia idara ya manunuzi ili ujenzi wa jengo hilo uweze kukamilika na kuanza kutumika.
"Nimeridhishwa na ujenzi unavyoendelea, DED (Mkurugenzi wa Halmashauri) isimamie idara ya manunuzi, wasikuvuruge, mkandarasi alipwe fedha zake, " alisema.
Akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Singida inayojengwa kwa Sh. bilioni 19.5 Waziri Mkuu, alisema ujenzi wa hospitali hiyo itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mkoa huu na mikoa jirani.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,(kushoto) akimpa mkono wa pongezi Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.