Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, ameongoza kwa mafanikio makubwa katika zoezi la ugawaji wa hati miliki za ardhi kwa wananchi wa vijiji vya Msungua na Mtunduru wilayani Ikungi, akisisitiza kuwa “Ardhi ni Maisha” na ni urithi halali wa vizazi vya sasa na vijavyo. Ameyasema hayo wakati akihutubia kwa wanakijiji waliojitokeza kushuhudia tukio hilo la kihistoria, RC Dendego alieleza kuwa serikali imeweka msukumo mkubwa wa kuhakikisha kila mwananchi anamiliki ardhi kihalali, hatua inayotatua migogoro na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Katika hotuba yake, Mkuu wa Mkoa alieleza kuwa hatima ya mizozo mingi duniani imejikita kwenye ardhi na rasilimali zake. "Ardhi siyo kitu kidogo, ardhi ni maisha kama ambavyo maji ni uhai," alisema kwa msisitizo, akitoa wito kwa wananchi kutunza hati walizopewa na kutambua thamani yake kama mtaji wa kifamilia na kimaendeleo.
Mhe. Dendego pia alitoa angalizo kwa vijana na wazazi, akiwataka kuacha tabia ya kuuza ardhi kiholela mara baada ya kupewa hati, kwani kufanya hivyo ni kuuza urithi na fursa za kiuchumi. Alisisitiza kuwa hati hizi ni kinga dhidi ya uvamizi, ni uthibitisho wa umiliki halali, na ni chachu ya uwekezaji wa kijamii na kifamilia
"Tumeweka maeneo ya akiba kwa ajili ya vizazi vijavyo, na mtu atakayevunja makubaliano hayo tutamshugulikia,” alionya.
Kwa upande wa wanawake, RC Dendego aliwahimiza kuchukua nafasi yao katika usimamizi wa ardhi ya familia na kuwa walinzi wa mali za familia, akisema, “Mama ni shingo, kichwa hakiwezi kugeuka bila shingo.” Alitoa rai kwa akinamama kuhakikisha matumizi ya ardhi yanapangwa kwa pamoja na kuhakikisha hati zinalindwa kama nyaraka muhimu za familia.
Aidha Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Shamimu S. Hoza, naye alieleza kuwa zoezi hilo ni sehemu ya mpango mkakati wa kufanya Singida kuwa kivutio bora kwa uwekezaji wa ndani na nje. Alisisitiza umuhimu wa kupanga matumizi bora ya ardhi kama silaha ya kukuza uchumi wa kaya, halmashauri na taifa.
"Ardhi inayopimwa inakuwa na thamani zaidi, na inamwezesha mwananchi kuwekeza kwa uhakika," alisema.
Naye Kiongozi wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kanda ya Kati, Bi Suzan Mapunda, alieleza kuwa mpango huu ni utekelezaji wa maelekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge iliyoitembelea Ikungi. Alibainisha kuwa tayari vijiji 44 vimepatiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi kati ya 101 ya wilaya hiyo.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila kijiji kina mpango wake, kila mwananchi anapata hati miliki yake, na tunapunguza kabisa migogoro ya ardhi,” alisema. ALiongeza kuwa hadi sasa zoezi limezaa jumla ya hati miliki za kimila 698 kwa vijiji vya Msungua na Mtunduru, ambapo 608 zilikamilika kwa ufanisi na kusambazwa kwa wananchi.
Wananchi waliopokea hati hizo walieleza furaha yao, wakisema hati hizo zimewaondolea hofu ya kuporwa ardhi, na kuwapa fursa ya kutumia ardhi yao kama dhamana ya mikopo au uwekezaji. Bi. Mugu Nyamwangi, mkazi wa Mtunduru, alisema: “Kuwa na hati miliki ni faraja kubwa, kwa sababu zamani tulikuwa tunaishi kwa hofu, lakini sasa tunajiamini. Naweza kutumia hati yangu kupata mkopo au kuwekeza.” Omary Husein aliongeza kuwa anajua sasa ardhi yake italindwa hata baada ya maisha yake, huku Fadhili Musa wa Msungua akisema kuwa hati hiyo ni ulinzi wa kweli dhidi ya wavamizi. Fatuma Ngarahe, mkazi wa Msungua, alieleza kwa furaha kuwa umiliki huo umempa heshima na ulinzi kama mama wa familia: “Hakuna tena atakayeninyanyasa wala kunibughudhi.”
Zoezi hili la ugawaji hati limechochea matumaini mapya kwa wakazi wa Ikungi. Kupitia dira ya Serikali ya Awamu ya Sita, pamoja na msukumo wa viongozi kama RC Halima Dendego, Singida inaendelea kuwa mfano wa utekelezaji wa sera bora za ardhi nchini. Wito mkubwa umetolewa kwa wananchi wote kuilinda ardhi yao, kuitumia kwa tija, na kuirithisha kwa vizazi kwa uwazi na mipango mizuri. Tukio hili limeashiria mwanzo mpya wa maendeleo ya ardhi katika Mkoa wa Singida, huku serikali ikionyesha dhamira ya dhati kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi kinapangwa, kinapimwa, na kumilikishwa kisheria – kwa ajili ya ustawi wa wananchi na taifa zima.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.