Baraza la Waislamu Tanzania(BAKWATA )Mkoani Singida wameandaa Kongamano la kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego kwa kazi kubwa na ushirikiano aliyouonyesha kwa Taasisi za dini, madhehebu yote ambayo yamekua ni kiungo muhimu katika kuwaunganisha Wanasingida pamoja na kuwa daraja la maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu,biashara ,ulinzi na usalama wa mali za wananchi na maadili kwa ujumla.
Tukio hilo limefanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwenge leo Jumamosi Januari 25,2025 likihudhuriwa na viongozi mbalimbali kama vile Mkuu wa wilaya ya Singida Mhe.Godwin Gondwe,Meya wa Manispaa ya Singida na wengineo.
Sheikh wa Mkoa wa Singida Issa Nassoro akizungumza wakati wa gafla hiyo ameainisha sababu mbali mbali za kumpongeza Mkuu wa mkoa wa Singida Mhe.Halima Dendego ikiwemo usimamizi wa uchaguzi Serikali za mitaa,kuongezeka kwa Mapato ya ndani kutokana na usimamizi bora,Pongezi kisekta katika sekta za Elimu katika Uandikishaji ,ufaulu wa Kidato cha sita,Kidato cha nne,Kidato cha pili na darasa la nne.
Sheikh Issa Nassoro amewaasa wanajamii kuwa na umoja kwa kushirikiana mambo mbalimbali ikiwa ni moja ya nyanja kuu ya kudumisha uhusiano mwema baina ya wanajamii kwa lengo la kudumisha ushirikiano na kuchochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Mkoa kwa ujumla.
"Maendeleo lazima kuzingatia Umoja, Huwezi pata Maendeleo bila umoja,wito wa Baraza Kuu la kislamu BAKWATA kwa wote ni kudumisha umoja ambao utatutoa hapa tulipo kwenda kwenye Maendeleo ,Umoja hauwezi patikana bila Mshikamano ili kuweza kufanikiwa"amesema Sheikh Issa.
Pia ametoa ombi kwa serikal kuwashirikisha viongozi wa dini katika kulinda na kujenga maadili kwa kushirikiana na Polisi Kata na watendaji pamoja na kuomba marekebisho ya Katiba ya mwaka 1999 huku akiwaonya watumishi kukosa ushirikiano, mshikamano na nidhamu kwa kutosikiliza maelekezo ya viongozi.
Naye Yohana Msita, Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida,Martha Mlata ,ametoa Pongezi kwa Viongozi wa Bakwata kwa kuendelea kuwa moja ya Taasisi za dini zinazoimarisha amani ya Mkoani Singida kwa kukemea vitendo viovu kwa jamii kupitia mafunzo mbalimbali.
Akitoa shukurani zake katika hafla hiyo,Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe.Halima Dendego amewashukuru Viongozi wa dini zote Mkoani Singida akisema kuwa tangu kufika kwake Singida wamekuwa walezi na washauri kwake na kusema kuwa pongezi hizo zimemtia moyo na kumpa hamasa ya kufanya kazi zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu suala la mmomonyoko wa maadili katika Mkoa wa Singida amebainisha moja ya sababu kubwa ya kuwa katikati ya nchi na kukutanisha watu wa jamii mbalimbali wenye tabia za tofauti, akisema kuwa mikakati mbali mbali imeandaliwa ikiwemo kushirikiana na vyombo vya dola kuchukua hatua mbalimbali za kimaadili.Pia kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali kuanzisha darasa la malezi kwa wazazi majumbani pia kutoa elimu ya dini na maadili kwa wanafunzi mashuleni.
Akizungumzia suala la uchaguzi Mkuu mwaka huu, ameomba wananchi kushiriki katika uchaguzi Mkuu mwaka 2025 kwa amani na utulivu kama walivyoshiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.