VIONGOZI na watendaji wa Halmashauri za Wilaya ya Singida wametakiwa kuweka mipango na mikakati bora ya maendeleo inayoendana na kiwango cha ongezeko la idadi ya watu katika maeneo yao iliyotokana na matokeo ya Sensa ya mwaka huu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 katika Wilaya ya Singida yaliyofanyika tarehe 8 Julai, 2023 kwenye ukumbi wa Sekondari ya Mwenge iliyopo Singida mjini Mkuu wa Wilaya hiyo Mhandisi Paskasi Muragili, amesema ongezeko la idadi ya watu iwe ni chachu ya maendeleo.
DC Muragili amesema Halmashauri zinatakiwa kuweka mipango bora ya kuwaendeleza na kuendeleza uzalishaji katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, afya, elimu, miundombinu, uchumi ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya watu.
“Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watu katika Halmashauri zetu zote mbili inazidi kuongezeka, hivyo kupitia mafunzo haya ni wajibu wa sisi viongozi na watendaji wote kwenda kupanga mipango thabiti”. Mhandisi Muragili
Amesisitiza kuwa wananchi wakiwa na uelewa mzuri wa matumizi ya matokeo ya Sensa ya watu na makazi itasaidia kutoa mchango wao katika maendeleo ya Taifa kwa kuwa watakuwa na uwezo sio tu wa kuishauri Serikali bali pia kupima utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya nchi na maeneo yao wanamoishi.
Katika hatua nyingine DC Muragili amepongeza juhudi za viongozi wa Wilaya ya Singida kwa kuwa maandalizi ya bajeti ya mwaka 2023/24 ya Halmashauri ya Manispaa na Singida DC yamezingatia matumizi ya matokeo ya Sensa na tafiti nyingine za kitakwimu zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
DC Muragili amehitimisha hotuba yake kwa kusema kuwa matumizi bora ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi, Majengo na Anwani ya Makazi ya Mwaka 2022 yataongeza umakini na ufanisi katika kutekeleza majukumu Serikalini na katika sekta Binafsi hivyo kuharakisha maendeleo kwa wananchi wa Singida.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga ametoa wito kwa waratibu wa Sensa wa Halmashauri za Wilaya mkoani Singida kusambaza matokeo ya Sensa ya mwaka huu katika ofisi zao ili takwimu hizo zianze kutumika hususan katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa maeneo husika.
Dkt. Mganga amesema Mkoa wa Singida umejipanga kuhakikisha mipango na programu zote za maendeleo zinapangwa kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi ya Mwaka 2022.
“Tumejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati na zenye ubora unaozingatia mahitaji halisi ya wananchi kulingana na idadi yao, jinsi yao, kuzingatia mahitaji maalum ya makundi mbalimbali katika jamii na hali ya mazingira wanamoishi” Dkt. Fatuma Mganga
Mkoa wa Singida kutokana na matokeo ya Sensa ya mwaka 2022 una idadi ya watu 2,008,058 kutoka watu 1,370,637 mwaka 2012 kati ya idadi hiyo watu 995,703 ni wanaume na watu 1,012,355 ni wanawake. Hivyo inaonyesha kiwango cha ukuaji wa idida ya watu imeongezeka katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kwa wastani wa asilimia 3.8 kikiwa zaidi ya wastani wa taifa ambao ni 3.2
Meneja Takwimu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mkoa wa Singida Naing'oya Kipuyo akisoma hotuba kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi na watendaji wa Wilaya ya Singida ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili, yaliyofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Mwenge Singida mjini tarehe 08 Julai 2023
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.