Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ameitahadharisha timu ya Yanga kuwa ijiandane kupambana na timu ya Singida United itakayocheza uwanja wa nyumbani ikiwa imara na tayari kwa ushindi kwa kuwa timu hiyo imeingia ligi kuu kushinda na sio kushiriki.
Dkt Rehema Nchimbi ameyasema hayo mara baada ya kukagua uwanja wa Namfua Stadium ambao mechi kati timu ya Singida United na Yanga itachezwa uwanjani hapo jumamosi hii huku akisisitiza kuwa timu ya Singida United imeingia Ligi kuu kushinda na sio kushiriki wala kufanya mazoezi.
"Yanga ijiandae kufungwa, kwetu ushindi ni muhimu kwakuwa tumejipanga sawasawa kwa ajili ya ushindi, hatujaingia Ligi kuu kushiriki au kufanya mazoezi, sisi tumeingia kushinda na Yanga walitambue hilo", amesisitiza Dkt Nchimbi.
Ameongeza kuwa ana uhakika wa ushindi kwa timu ya Singida United kutokana ana ubora na maandalizi mazuri ya timu pamoja na kuchezea uwanja wa nyumba wa Namfua ambao umeboreshwa kwa viwango vya hali ya juu.
"Kwa mara ya kwanza baada ya miaka kumi na saba timu yetu itacheza mechi ya ligi kuu katika uwanja wa nyumbani, Uwanja huu ambao ni mali ya Chama cha Mapinduzi umekarabatiwa na uko katika hali bora sana", ameeleza Dkt Nchimbi.
Aidha amewataka mashabiki wote wa Singida United waliopo mkoani Singida na mikoa ya Jirani kujitokeza kwa wingi ili kutoa hamasa na kuishangilia timu yao pamoja na kushuhudia ikifanya vizuri.
Ameongeza kuwa katika mechi hiyo kutakuwa na fursa za kufanya biashara mbalimbali hivyo amewataka wafanyabiashara wote kupeleka bidhaa bora ambazo zitautangaza vema mkoa wa Singida.
Kwa upande wake Katibu wa Timu ya Singida United Abdulrahman Sima amesema timu hiyo imeshawasili mkoani Singida kwa ajili ya mechi ya jumamosi huku wakitarajia ushindi kutokana na mazoezi pamoja na hamasa ya mashabiki wake watakaojitokeza katika uwanja wa Namfua.
Sima amesema kuwa maandalizi yote yako tayari huku ukarabati wa uwanja, vyoo na vyumba vya wachezaji vikiwa katika hali nzuri, mageti yote yako imara na pia shirikisho la Mpira wa miguu nchini (TFF) wameshafanya ukaguzi wa uwanja huo.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.