Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Daktari Fatuma Mganga amewaasa watumishi kuweka mbele maadili ya utumishi wa umma katika kutoa huduma sambamba na kujituma kwa bidii ili kuwaimarisha katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya sheria, uwazi na uwajibikaji ili kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi za serikali.
Daktari Mganga ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo juu ya Rushwa kwa Watumishi wa Umma yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida leo Mei 27,2025 ambapo Mafunzo hayo yametolewa na Afisa wa TAKUKURU Mkoa wa Singida na yaliyohudhuriwa na Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Singida.
Awali Dkt. Fatuma Mganga amewasistiza Watumishi wote kuwa na mwenendo mzuri ambao utawanufaisha wananchi bila kudhulumu haki zao na wafanyakazi wenzake.Kadhakika ameongeza kuwa Watumishi wa Umma wote wanatakiwa kujikumbusha Kila mara kuhusu maadili ya kazi na maelekezo ya namna ya kufanya kazi walizoajiwa nazo huku akiwataka Watumishi wa Umma wote kujitathmini na kubadilika baada ya kupata mafunzo hayo kwa manufaa ya nchi na wananchi wote.
"Rushwa si suala la kutoa ama kupokea fedha ama kitu bali hata uchelewaji na kutokufanya kazi kama ipaswavyo au Serikali ivyokutuma kufanya, Wengine huenda wakawa wanafanya vitendo vya Rushwa bila kujua hivyo tunapaswa kuwasikiliza wataalamu hawa ili tuweze kujitafakari vizuri katika maadili ya kazi zetu kadhalika yapasa tuwe na tabia ya kuripoti matendo hayo ya Rushwa bila woga, na kutoa Ushirikiano wa dhati na ushahidi unaohitajika katika kitengo cha TAKUKURU".amesema Daktari Mganga.
Naye Afisa wa TAKUKURU mkoa wa Singida,Bw.Onesmo Mdegela akitoa mafunzo haya,amesistiza kuwa Watumishi wazingatie maadili na kuwa na Staha katika kazi pamoja na kuzingatia haki za wafanyakazi na wananchi kadhalika na kuepukana na mitego mbalimbali wanazoweza kuingia bila kufahamu ikiwemo kupokea zawadi
"Tuepuke kupokea zawadi kutoka kwa watu tunaowahudumia,zawadi sio Rushwa lakini inakuweka kwenye mgongano au ukinzani wa nafasi na maslahi ambayo husababisha upendeleo na pia kwenda kinyume na sheria za nchi na hatimaye kuingia kwenye mkondo wa Rushwa. Serikali imeweka mfumo kuwa ukipokea zawadi usiitumie, iwasilishe kwa kiongozi, wako ndipo apange matumizi"
Bw. Mdegela,amefundisha pia nadharia za maadili ikiwemo nadharia ya maadili ya matokeo ambayo hupimwa kutokana na utendaji kazi na matokeo ya utendaji ya mtumishi husika ambayo hupimwa kwa uzalendo bila kuangalia masilahi binafsi kwa kuzingatia manufaa ya wengi pamoja na nadharia ya maadili ya uwajibikaji kwa watumishi kufanya kazi kwa namna ambayo wengine watajifunza kutoka kwako kwa kuwa mfano wa kuigwa ikiwemo suala la kuzingatia muda.
Kadhalika amewaasa watumishi kutokuwa na hofu ya kuripoti vitendo mbalimbali vya kuombwa rushwa ikiwemo Rushwa ya ngono ambayo wengi wanapata uoga wa kuiripoti,sambamba na kufanya kazi kwa uaminifu na kujituma na ufanisi bila kusukumwa,kufanya kazi kwa taaluma husika,kusimamia fedha za umma vizuri,kujali mipaka ya kazi kwa kuwa na maisha binafsi yenye heshima mambo ambayo yatawaepusha na kujiingiza katika vitendo vya kuomba au kupokea rushwa.
Bw.Fredrick Ndahani,Afisa Vijana kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida akizungumza baada ya mafunzo hayo,amesema kuwa amejifunza kuwa muwajibikaji kwa kufanya kazi kwa kujituma zaidi ili kujiweka mbali na mambo yanayotoa mwanya wa rushwa,kadhalika kutoa huduma bora na za kuridhisha kwa jamii ili kuwapa huduma bora wanazostahili.
Mafunzo hayo yanalenga na kuwakumbusha Watumishi wa Umma watumie mamlaka yao vizuri na wasipende kutumiwa ama kutumika vibaya,kadhalika kuwa na utambulisho mzuri katika jamii zao kwa kuhakikisha wanakua na staha,utu na matendo mema ili kuijengea heshima kazi,Taasisi na jina la mtumishi binafsi.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.