Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego amewashauri wahitimu wa taasisi ya Uhasibu Tanzania kufikiri zaidi kujiajiri badala ya kutegemea ajira za serikali na sekta binafsi.
Mhe.Dendego amesema hayo katika mahafali ya 22 ya chuo cha Uhasibu Tanzania tawi la Singida. , na mahafali ya 13 ya Tawi la Singida, yaliyofanyika chuoni hapo kuanzia ngazi ya cheti hadi uzamili.
“ Nawaomba mfikirie zaid kujiajiri kuliko kuajiriwa vipaji mnavyo kama nilivyoona wanafunzi wakibuni mbinu mbalimbali za biashara kwani licha ya ajira kutoa fursa nzuri lakini kujiajiri kunatoa nafasi ya kuwa mbunifu na uhuru wa kufikia malengo yaliyokusudiwa"alisema Mhe.Dendego.
Akiongelea kuhusu wahitimu 1477 waliohitimu katika fani mbalimbali amesema idadi hiyo ni kubwa na faraja kubwa kwa Mkoa wa Singida hivyo wakiitumia katika kutengeneza ajira kutaleta mabadiliko
Kuhusu baadhi ya wanachuo wanao onyesha ubunifu, Mkuu wa Mkoa amesema serikali ya mkoa itashirikiana nao kwa karibu ili kuhakikisha wanafikia malengo yao huku akiwataka kutumia mitandao ya kijamii kama jukwaa la kutangaza ubunifu, kukutana na wateja, na kueneza mawazo mapya Badala ya kupoteza muda mitandaoni kwa mambo yasiyokuwa na manufaa kwani mitandao hiyo inatoa fursa kubwa ya kujitangaza, kukuza biashara, na kufikia mafanikio makubwa.
Awali,Mhe. Dendego alianza kwa kuzindua program ya ‘Masters’ ambayo itapatikana katika kampasi ya Singida huku akipongeza juhudi zinazofanywa na Taasisi ya Uhasibu Nchini (TIA), katika kuboresha miundombinu na kusimamia maendeleo ya Tawi lake la Singida, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo jipya la utawala litakalokuwa na ghorofa tano na kugharimu zaidi ya Shilingi bilioni 13.5.
Ameeleza kuwa maboresho hayo yanaashiria ukuaji wa chuo hicho na yanaongeza fursa kwa vijana kujifunza maarifa na ujuzi zaidi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
“Serikali itaendelea kushirikiana na wanafunzi na uongozi wa chuo hiki. Nawaomba sana mkitumie chuo hiki kujipatia maarifa zaidi kwa ajili ya kuitumikia jamii katika kila nyanja,” alisema Dendego.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Palangyo, alisema kuwa kuanzishwa kwa shahada ya uzamili katika Tawi la Singida ni hatua muhimu itakayochochea ongezeko la wanafunzi wanaotamani kujiunga na chuo hicho.
“Hadi sasa, tayari tumewasajili wanafunzi 66 kwa shahada ya uzamili, ambao wanaendelea kupata maarifa na ujuzi zaidi kwa manufaa yao binafsi na ya taifa kwa ujumla,” alisema Profesa Palangyo.
Naye Mjumbe wa Bodi ya TIA, Renatus Msangira, aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Bodi hiyo, aliwahimiza wananchi kutumia fursa ya uwepo wa chuo hicho kwa kuongeza maarifa ambayo yataboresha maisha yao.
Jumla ya wahitimu 1,477 walitunukiwa vyeti vyao katika ngazi mbalimbali za masomo, zikiwemo cheti na stashahada kwenye fani za mahusiano ya umma, uhasibu, uongozi wa rasilimali watu, usimamizi wa biashara, pamoja na ununuzi na ugavi.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.