Halmashauri za Mkoa wa Singida zimepongezwa kwa kupata hati safi katika mwaka wa fedha unaoishia Julay 2022 baada ya ukaguzi uliofanywa mwaka 2022/23 na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akiwa katika kikao kazi kilicho wahusisha wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Tarafa pamoja na Maafisa elimu.
Wakiwa katika kikao hicho RC Serukamba amewaeleza Wakurugenzi kwamba wahakikishe hakuna fedha mbichi inayotumika kabla ya kuingizwa benki ikiwa ni maagizo yaliyotolewa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan huku RC Serukamba akikemea tabia ya wakusanya mapato kukaa na fedha za Serikali zaidi ya siku mbili pasipo kuipeleka benki.
Aidha amewaagiza Wakurugenzi hao kuhakikisha wanafuata sheria katika kutenga na kutumia fedha za mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya mikopo ya wanawake vijana na walemavu na kuzisimamia mikopo hiyo ili iweze kurejeshwa kwa wakati.
Hata hivyo amewakumbusha Wakuu wa Wilaya kwenda vijijini na kukutana na wazazi lengo likiwa ni kuwahamasisha kujitolea katika ujenzi wa shule katika maeneo ambayo madarasa hayapo ya kutosha kama sehemu ya kuanzisha miradi mipya ya Halmashauri.
Amesema anataka zoezi la usajili wa wanafunzi lifikie asilimia zaidi ya 90, kwenye programu za Lishe Wakurugenzi wahakikishe kwenye kadi alama hakuna rangi ya njano wala nyekundu na kwenye ufaulu anataka ifikie asilimia zaidi ya 90.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga amewataka Wakurugenzi na Maafisa Elimu kuhakikisha ufaulu unaongezeka mpaka kufikia asilimia 90 huku akibainisha kwamba hatapenda kuona daraja sifuri na ikiwezeka ufaulu uishie daraja la tatu.
Hata hivyo amesisitiza viongozi hao kujipanga kuondoa utoro kwa wanafunzi kwa sababu ndio unasabibisha ufaulu mdogo au kufeli kwa wanafunzi huku akisistiza kuimarishwa programu ya chakula mashuleni.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.