Jopo la Mawaziri Wanane na makatibu wakuu kutoka wizara za kisekta wametembelea vijiji Kumi na mbili (12) mkoani Singida vyenye migogoro ya ardhi ili kutathimini na kupendekeza namna ya kumaliza migogoro hiyo.
Akiongea leo tarehe 8 Oct. 2021 wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa mkuu wa Mkoa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi amesema Timu hiyo iliyoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano itatembelea vijiji 920 vyenye migogoro ya ardhi katika Mikoa 10 ambapo 12 na viwili vipo mkoani Singida.
Amesema lengo la timu hiyo ni kuhakikisha wanatatua migogoro hiyo iliyoripotiwa awali na kuhakikisha inakwisha pasipo kuleta taharuki ambapo pia mipaka itawekwa ili kuwasaidia wananchi.
Amesema katika migogoro ya ardhi au ile ya wakulima na wafugaji imekubalika na Baraza la Mawaziri kwamba Muungano huo wa wizara za kisekta ndio utakao tumika kutatua migogoro ya namna hiyo badala kila wizara kwenda yenyewe.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akishukuru timu hiyo amesema Mkoa utatoa ushirikiano kuhakikisha tathmini hiyo inakamilika na wananchi wanaendelea kuishi katika maeneo hayo.
Amesema maeneo yenye migogoro ya ardhi ni Wilaya ya Iramba, Singida, Ikungi na Manyoni na kuomba maeneo ambayo yana mgogoro na baina ya Jeshi na wananchi na ambayo Jeshi haliyatumii busara zitumike wapewe wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge alisema, Ofisi yake sasa itahakikisha inasimamia pamoja na kuifatialia migogoro yote ya ardhi ikiwemo ile ya mipaka katika wilaya na vijiji ili kumaliza kabisa migogoro ya ardhi.
Wakiwa katika Manispaa ya Singida Mawaziri hao wametembelea eneo la Mwankoko lenye mgogoro ulioanza mwaka 2016 kati ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini hapa (SUWASA) na wananchi wanaolalamikia kupunjwa fidia waliyolipwa na Serikali ili kupisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Mwankoko ambapo baada ya Mawaziri kusikiliza pande zote mbili, Mwenyekiti wa Kamati wa Mawaziri wa Kisekta ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Wiliam Lukuvi amemwagiza Mthamini Mkuu wa Serikali kufika mkoani hapa siku ya Jumatatu tarehe 11 Oct. 2021 ili kufanya uchunguzi na kujua ukweli kuhusu malalamiko hayo.
Mawaziri hao wa kisekta waliokuwa kwenye ziara hiyo ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, TAMISEMI, Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Mazingira, Utalii, Ulinzi na Maji.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.