WAKUU wa Wilaya mkoani Singida wametakiwa kujenga utaratibu wa kutatua migogoro mbalimbali katika jamii ili wananchi waendelee kuwa na amani na imani na Serikali yao.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, ametoa rai hiyo jana Februari 20, 2023 katika mkutano wa kupokea kero za wananchi uliofanyika katika shule ya Sekondari Ilongero, iliyoko mkoani hapa.
“Nawaomba Ma-DC mjenge utaratibu wa kutatua kero za wananchi, wana vijiji hawa ni watu wetu, hawa ndiyo wamekichagua Chama chetu (CCM), tukitatua changamoto za wana vijiji wetu watakipenda chama chetu, watampenda Rais wetu (Mama Samia Suluhu Hassan), watampenda Mbunge, DC na viongozi wetu wote,” alisema.
Katika hatua nyingine Serukamba amempa wiki moja kuanzia Mkuu wa Wilaya Singida, Mhandisi Paskasi Muragili, kumaliza mgogoro wa ardhi wa muda mrefu katika shule ya Sekondari Ilongero.
Wakati wa kikao hicho wananchi walimwambia Serukamba kwamba mtu mmoja analima na kupanda mazao katika eneo la eka nne la shule hiyo akidai kuwa ni lake licha ya kuwa alikuwa ni mmoja wa waliohamishwa kupisha ujenzi wa shule hiyo tangu miaka 1980.
Serukamba ameagiza kuwa mvamizi huyo aachwe avune mazao yake na hatimaye aliache eneo hilo na kwamba DC Muragili pamoja na ofisa ardhi mkoa wahakikishe katika kipindi hicho wanapima eneo hilo kumaliza mgogoro huo.
Pia ametoa wito kwa makatibu Tarafa kuwasimamia viongozi wa Serikali za vijiji ili wasiwe sababu ya migogoro ya ardhi badala yake wawe watatuzi.
Awali akizungumzia mgogoro wa shule hiyo, Diwani wa Kata ya Ilongero, Issa Juma, alisema upo tangu miaka ya 1990 na kwamba mtuhumiwa huyo amekuwa akilima eneo hilo licha ya kuaswa na viongozi kwa nyakati tofauti kuwa aliache.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo wa kusikiliza na kutatua kero.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.