MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amewagiza Maafisa manunuzi na Wahandisi wa Wilaya ya Mkalama mkoani hapa kujipanga vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao ili kutozalisha hoja za ukaguzi ambazo zimekuwa zikiibuliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Moses Machali, kwenye kikao maalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo alisema hoja nyingi za CAG zimekuwa zikijitokeza kwenye idara ya manunuzi na wahandisi hivyo kama watumishi katika idara hizo watajipanga vizuri katika kutekeleza majukumu yao vizuri hakutakuwa na hoja za ukaguzi kila mwaka.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Moses Machali, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida kwenye kikao maalum cha Baraza la Madiwani.
Alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wapo baadhi ya watumishi wanakwamisha utendaji kazi na wengine wanatekeleza vizuri majukumu yao hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kutekeleza majukumu yake vizuri ili hoja za CAG zisiwe zinajitokeza kila mwaka.
Alisema ni aibu kila mwaka kuibuka kwa hoja za CAG ambazo nyingine zinasababishwa na uzembe wa watendaji na kwamba wakati umefika sasa kwa kila mtendaji kuwajibika ipasavyo ili hoja za CAG zisiwe zinajitokeza kwenye Halmashauri.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga, akizungumza kwenye kikao maalum cha Baraza la Madiwani.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida (RAS), Dkt. Fatma Mganga, alisema Mkoa wa Singida umetajwa katika mikoa mitano ambayo ina hoja nyingi za CAG ambapo ulikuwa na hoja 489 lakini sasa baadhi zimefungwa na kubakia hoja 239.
Alisema kutokana na changamoto hiyo suala la kushughulikia hoja za CAG liwe endelevu kwenye vikao vya Kamati za Fedha na Uongozi ambavyo vinafanyika kila mwezi.
Dkt. Mganga aliwataka Madiwani kuwasimamia watendaji ili kupunguza hoja hizo za CAG na kwamba hakuna sababu ya kila mwaka kuwa na hoja nyingi hali ambayo inasababisha watendaji kuona ni kama jambo la kawaida.
Alisema kasi ya kujibu hoja katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama sio ya kuridhisha sana kwani ilikuwa na hoja chache 51 lakini zilizofungwa kipindi hiki ni 24 na kubakiwa na hoja 27 ukilinganisha na Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ambayo ilikuwa na hoja nyingi 113 ambayo hadi sasa imefunga hoja 80 na kubakiwa na hoja 33 tu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Jamse Mkwega, akizungumza kwenye kikao maalum cha Baraza la Madiwani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, alisema wataalam wawe wanasimamia miradi vizuri iwe inajengwa kwa kiwango kinacholingana na thamani ya fedha na hivyo kuwarahisishia Madiwani wanapoikagua wafanye kazi ya kuwapongeza tu.
Alisema watumishi wajipange kusiwe kunazalishwa hoja za ukaguzi kwani nyingine zinakuwa hazina msingi kuwepo kwani baadhi ni suala tu la kukosekana kwa nyaraka.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Moses Machali, akisisitiza jambo wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. Asia Juma Messos akizungumza kwenye kikao maalum cha Baraza la Madiwani.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.