Mkoa wa Singida unatarajia kuwa na kliniki ya madaktari Bingwa wa magonjwa mbalimbali wajulikanao kama MADAKTARI BINGWA WA DKT SAMIA" yatakayofanyika mwezi Mei ,2025 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida iliyopo kata ya Mandewa.
Hayo yamezungumzwa katika kikao cha tathmini na maandalizi ya kupokea huduma hiyo kilichofanyika leo Februari 28,katika ukumbi wa NAO kikiongozwa na Katibu Tawala Mkoa Wa Singida,na kushirikisha Wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa za Mkoa wa Singida,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida,Waganga wakuu wa Halmashauri ,Timu ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na RHMT.
Katika zoezi hilo wanatarajia kuwa na huduma za kibingwa na huduma bobezi ikishirikisha madaktari bingwa kutoka hospitali za rufaa za mikoa ya Dodoma, Morogoro, Pwani,Iringa na Kanda ya Benjamin Mkapa na wenyeji Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.
Madaktari hao watatoa huduma mbalimbali ikiwemo kutibu magonjwa ya ndani,magonjwa ya wanawake na uzazi,magonjwa ya watoto,upasuaji,upasuaji wa mifupa,magonjwa ya njia ya Mkojo, macho,sikio,pua na koo,upasuaji na urekebishaji wa kinywa na meno,huduma ya Radiolojia,usingizi na ganzi,utengamano na viungo(fiziotherapia),upasuaji wa mishipa ya fahamu na ubongo,Ngozi,afya ya akili na huduma za kutibu makovu mbali mbali.
Katika zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika kwa siku tano,Mkoa unategemea kutoa huduma kwa takribani wananchi 3000 kwa siku tano huku taratibu za malipo za kawaida zikitumika pamoja na huduma ya msamaha kwa baadhi ya wananchi ambao hawatakuwa na uwezo.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Daktari Fatuma Mganga, akizungumza wakati akipokea taarifa hiyo amesema ni vema kutumia nafasi kubwa ya uhamasishaji na kuutaarifu umma kuhusu ujio wa Madaktari hao Mkoani hapa kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanajitokeza kwa wingi na kunufaika na matibabu hayo.Pia ameshauri wananchi kuhimizwa kukata Bima za Afya kwa wale ambao hawana kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo.
Awali Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Singida,Dkt David Mwasota,aliwasilisha changamoto zilizotarajiwa kuwepo ikiwemo ufinyu wa Shemu za kutolea huduma na mizunguko mirefu kwa wateja,huku akisema kuwa changamoto hiyo imefanyiwa utatuzi kwa kuongeza vituo vya kutolea huduma ikiwemo baadhi ya vyumba vya wodi ya watoto na jengo la One Stop Centre.Pia matumizi ya mahema katika kutoa huduma ya consultation(kumuona daktari),kuongeza sehemu za malipo na vituo vya kukusanyia Sampuli za maabara.Pia ametoa ombi kwa uongozi wa Mkoa na Manispaa kukamilisha ukarabati wa vyumba vya upasuaji hospitali ya Manispaa ili kuweza kutumika katika zoezi hilo.
Zoezi hilo linakwenda sambamba na Kauli mbiu isemayo; "Madaktari Bingwa wa Dkt.Samia-Karibu Tukuhudumie".
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.