KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 , Godfrey Mnzava, ameiagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijiji (RUWASA) kuweka utaratibu wa kuziwezesha Jumuiya za Watumia Maji kifedha na mafunzo ili ziweze kutunza vizuri raslimali maji na miundombinu na hivyo kudumu muda mrefu kutoa huduma za maji kwa wananchi kwa kiwango bora.
Ametoa agizo hilo leo (Julai 6, 2024) wakati wa kuzindua mradi wa maji katika kijiji cha Mabondeni Halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni Mkoani Singida ambao umegharimu Sh.milioni 280 ambao utahudumia zaidi ya wananchi 2500.
Mnzava amesema serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kujenga miradi ya maji ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama hivyo miundombinu ya miradi hiyo inatakiwa kutunza vizuri ili iendelee kutoa huduma hizo na jukumu hilo linapaswa kufanywa na Jumuiya za Watumia Maji.
Amesema pia wananchi wanapaswa kutunza vyanzo vya maji visiharibiwe kwani vyanzo vya maji vikiwepo vitaongeza upatikanaji wa maji na hivyo kuondoa kero ya upatikanaji wa maji kwa wananchi kama ilivyo dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muunganow wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusogeza huduma za maji kwa karibu kwa wananchi.
Aidha, Mnzava ambaye aliridhia mradi huo na kuuzindua ameipongeza RUWASA kwa kutekeleza vyema mifumo ya manunuzi ya umma hali ambayo imesaidia kupunguza malalamiko kwamba wapo baadhi ya wakandarasi wanapendelewa kupewa zabuni za kujenga miradi ya maji.
Awali Meneja wa RUWASA Wilaya ya Manyoni, Mhandisi Gabriel Ngongi, akitoa taarifa ya mradi huo amesema mradi huo uliibuliwa na wananchi mwaka 2022 kwa nia ya kupunguza tatizo la ukosefu wa maji.
Amesema ujenzi wa mradi huo ulianza Agosti 1,2023 na kukamilika Juni 15, 2024 ambapo una kisima chenye uwezo wa kuzalisha maji lita 4,000 kwa saa.
Ngongi amesema ujenzi wa mradi huo ulikadiriwa kutumia kiasi cha Sh. 280,800,000 ikiwa ni fedha kutoka Serikali kuu kupitia Programu ya malipo kwa Matokeo (P4R) lakini hadi kukamilika mradi umetumia kiasi cha Sh. 275,880,099.72.
Amesema fedha hizo zimetumika kujenga Pump House, uunganishaji Mfumo wa umeme, kununua na kufunga mitambo ya kusukuma maji, ujenzi wa mtandao wa bomba, ujenzi wa Tenki la maji la lita 54,000 kwenye mnara wa meta 12 pamoja na Ujenzi wa vituo 5 vya kutolea huduma ya maji.
Meneja huyo amesema faida za mradi huo ni pamoja na kuboresha kipato cha wananchi kwa kutumia muda mfupi wa kupata maji safi na salama kwa gharama nafuu na hivyo kutumia muda mwingi uliobakia kwenye shughuli za uzalishaji, kuboresha afya za wakazi wa kijiji cha Mabondeni.
Faida nyingine ni kujenga mazingira mazuri ya wanafunzi kujisomea badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji atokapo shuleni na kupungua kwa kero kwa viongozi itokanayo na Malalamiko ya kila siku ya ukosefu wa maji safi na salama.
"Sisi Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, hususani Kijiji ya Mabondeni kwa heshima kubwa tunamshukuru sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuletea fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu. Tumeona nia ya dhati ya Serikali Kumtua mama ndoo ya maji kichwani na tunaahidi kutunza mradi huu ili uendelee kuinufaisha jamii na kwa maendeleo endelevu".
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.