Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge leo Desemba 1, 2021 ameshiriki utiaji wa saini katika mikataba 26 ya awamu ya pili baina ya Wakandarasi na Wakala wa barabara za vijijini na mijini TARURA wa mkoani hapo zenye thamani ya Sh. Bilioni 12.6 ambazo zimetokana na makusanyo ya tozo za miamala ya simu.
Utiaji saini huo umefanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa pamoja na taasisi za kifedha zikiwemo benk ya CRDB, NMB na makampuni ya bima kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kuwakopesha Makandarasi hao.
Akiongea katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa akawataka Makandarasi waliopata kazi hizo za utengenezaji wa barabara katika Halmashauri saba (7) za Mkoa wa Singida akawataka kuhakikisha kwamba zinajengwa kwa viwango ili kulingana na thamani ya fedha zinazotolewa.
Aidha RC Mahenge akawakumbusha Wakandarasi hao kutumia ratiba ya kazi vizuri na kukamilisha kazi kwa wakati huku akiwataka kutumia muda huu ambapo mvua sio nyingi kuanza na utekelezaji wa miradi kwa sababu hakutakuwa na muda wa nyongeza.
“Kwa kuwa fedha zinazotumika ni kodi za wananchi zinazotokana na makato kweye simu ni vizuri kila mmoja wenu afanye kazi kwa uzalendo kwa kuwa miradi yote inatekelezwa na makandarasi wazawa, tuhakikishe fedha zinatumika kulinga na kazi zinazofanyika”. alifafanua Dkt. Mahenge.
“Kupata mradi ni jambo moja na kutekeleza mradi ni jambo la pili, nafahamu wapo watu watatumia zaidi ya siku 14 walizopewa za kukusanya vitendea kazi kwa mambo mengine hivyo kusababisha ucheleweshaji wa kazi, hatutakuwa na msamaha kwa mkandarasi yeyote atakaye fanya kazi mbaya na atakayechelewesha kazi”. Aliendelea kusisitiza Dkt. Mahenge.
Hata hivyo Dkt. Mahenge akatumia muda huo kuishukuru Serikali kwa kutoa Bilioni 12.6 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mijini na vijijini katika wilaya zote mkoani Singida na kukiri kwamba kwa kipindi kifupi kilichopita walipata Sh. Bilioni 27 za UVIKO 19 ambazo zililenga kwenye miradi ya maendeleo hivyo kwa kipindi kifupi Serikali imeleta fedha nyingi kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali mkoani hapa.
Akimaliza hotuba yake RC Mahenge akawashukuru TARURA kwa jitihada zao za kufanikisha mchakato wa kuwapata Wakandarasi wenye sifa zinazukubalika hivyo kuwataka wakala hao wa barabara za vijijini na mijini kuwasimamia ili waweze kukamilisha kazi kwa wakati na kwa kiwango kinacho stahili.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa Jumanne Kilimba amesema kupitia kamati ya siasa watahakikisha wanakagua miradi hiyo kwa umakinifu mkubwa ili kuhakikisha wananchi wanapata kile kilicho tarajiwa kufikishwa na Serikali kwa lengo la kuwanufaisha wakazi wa Mkoa wa Singida.
Hata hivyo amebainisha kwamba Wakandarasi hao wana uwezo mkubwa kwa kuwa wengi wao wameshafanya kazi mkoani hapo na kuwahakikishia kwamba wanaendelea kupata kazi mkoani hapo endapo watafanya vizuri na kuwakumbusha kwamba atakaye haribu Mkoa wa Singida asitegemee kupata kazi mkoa wowote.
Awali akieleza malengo ya hafla hiyo Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Tembo D.R amesema mikataba hiyo itatekelezwa katika Wilaya ya Iramba, Itigi, Singida DC, Manyoni Mkalama, Ikungi na Manispaa ya Singida.
Amesema makampuni yaliyopata kazi hizo ni M/S Kangwa General Supply Ltd, M/s J.P Trader Ltd, Chase Investment, Brand Mark, Kumba Quality, Sumaco Eng., Coyesa company, Gornad company na nyinginezo nyingi ambazo kwa mujibu wa mkataba wanatakiwa kumaliza kazi ndani ya miezi 6. Alifafanua Mhandisi Tembo.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.