Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani Singida wameaswa kununua vifaa mbalimbali vya ujenzi kwa wafanya biashara wa ndani ya Mkoa huo hasa kipindi hiki ambacho Serikali inajenga vyumba vya madarasa chini ya miradi wa boost ili kuwanufaisha wafanya biashara.
Maagizo hayo yametolewa tarehe 18.05.2023 na Mkuu wa Mkoa huo, Peter Serukaba wakati akikagua ujenzi wa miradi ya shule katika Manispaa ya Singida ambapo alieleza kwamba miradi hiyo itawanufaisha wafanyabiashara endapo vifaa vya ujenzi vitanunuliwa kwao.
Aidha, amekemea baadhi ya viongozi ambao katika Manispaa ya Singida wameshindwa kuendelea na ujenzi wa moja ya shule katika Manispaa hiyo kwa kile walichodai kwamba wameagiza nondo Dar es Salaam na zilikuwa bado hazijafika wakati ujenzi unatakiwa kukamilika kabla ya tarehe 30.6.2023.
"Tulikubaliana kwamba vifaa vyote vinunuliwe hapa ndani ya mkoa ili kuwanufaisha wafanyabiashara wa ndani na kuwapatia ajira za muda mfupi mafundi wa maeneo husika" Serukamba
Hata hivyo amewataka Viongozi hao kutumia muda wao mwingi kwenye usimamizi wa miradi hiyo ili kuhakikisha hakuna fedha itakayorudi wakati wananchi wana uhitaji mkubwa wa shule hizo.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya, Mhandisi Paskasi Muragili alibainisha kwamba vifaa vya ujenzi vinavyopatikana hapa Singida vina ubora mzuri ambapo ameeleza kwamba vifaa kwenda kununuliwa nje ya Mkoa huo kunaleta maswali mengi na kinaendelea kuchelewesha mafundi kuendelea na kazi.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa hiyo, Yagi Kiaratu amesema wamepokea maelekezo ya Mkuu wa Mkoa na watahakikisha kila Mkuu wa Idara au Kitengo anapata mradi mahsus na kuusimamia lengo likiwa ni kumaliza kwa wakati na kwa viwango.
Ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa imefanikiwa kutembelea miradi 12 ya ujenzi wa vyumba vya madarasa Kituo cha Afya, Zahanati na bweni la Sekondari.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.