Jumla ya mitungi ya gesi ya Nishati safi ya kupikia elfu ishirini na tisa (29,000/=) imetolewa kwa bei ya ruzuku leo, Majiko hayo yakiwa ni mwanzo wa kwenda kufikia kaya zote za Mkoa wa Singida takribani kaya laki tatu na nusu .
Majiko hayo yametolewa leo katika kilele cha siku ya Mwanamke duniani ambapo Mkoa wa Singida wameadhimisha leo kimkoa katika uwanja wa Bombadia ulipo Manispaa ya Singida na Mgeni rasmi akiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego.
Mheshimiwa Dendego amesema kuwa Wizara ya nishati kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika mpango wake wa upatikanaji wa Nishati safi Vijijini wametoa majiko hayo ikiwa ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa nishati safi, lengo lake ni kuhakikisha kaya zote zinapata nishati safi ya kupikia.
Amesema kuwa Majiko hayo ni ya kilo sita ambapo dukani yanauzwa kati ya shilingi elfu arobaini mpaka elfu arobaini na tano lakini yameuzwa kwa ruzuku ya elfu ishirini na mia nane ,(20,800)ambapo baada ya majiko hayo yatasambazwa katika halmashauri zote mkoani Singida na kuwafikia wananchi wote wa mijini na vijijini.
Akizungumza baada ya kupata mtungi wa gesi leo,Amina Mwaju mkazi wa wilaya ya Iramba ameonyesha kufurahia kupata nishati safi hiyo kwa bei ya riziki ambayo anasema kubwa hakutegemea angepata kwa bei nafuu.
"Kwa kigezo cha kuwa na kadi ya NIDA pekee ,leo nimekuwa miongoni mwao wanufaika wa kutumia nishati safi kwa gharama ndogo sana ambayo mwanzoni nilishindwa kuipata kwa sababu ya gharama kubwa juu,lakini sasa nimefurahi kwani itanisaidia kwa mambo mengi hususani kupika kwa muda mfupi huku nikipata muda mwingi katika uzalishaji rasilimali nyingine tofauti na ilivyokuwa hapo mwanzo nikitumia kuni"amesema Bi Mwaju.
Kilele cha maadhimisho ya siku ya Mwanamke kimkoa wa Singida yamefanyika leo 7/3/ 2025 ambapo yalianza na maandamano kutoka ofisi ya mkuu wa Mkoa na kuelekea katika uwanja wa Bombadia ambapo maonyesho na Burudani mbalimbali zimefanyika pamoja na ugawaji wa tuzo huku Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan akipokea tuzo ya heshima kutoka kwa wanawake wa Singida, lengo la siku hii likiwa ni kufurahia ,kutathimini na kupongeza juhudi za kujikwamua kiuchumi na kimaendeleo kwa ujumla kwa Wanawake.
Lengo la Siku ya Mwanamke duniani kuadhimishwa rasmi tarehe 8 Machi kila mwaka ni kutumika kama siku rasmi ya kuikumbusha dunia juu ya haki za wanawake.Siku hii pia huongeza chachu katika harakati za mapambano katika usawa wa kijinsia kwa wanawake na wanaume katika jamii.
Kwa mwaka huu siku ya Mwanamke duniani kitaifa itafanyika Mkoani Arusha Machi 8,2025 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan na Kauli mbiu ya Mwaka huu ni "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki,Usawa, na Uwezeshaji,"
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.