Mwenge wa uhuru leo umezindua rasmi mkakati wa kuboresha sekta binafsi mkoani Singida kwa kuwa na madawati ya kuratibu sekta hizo ili kufikia uchumi wa kati wenye viwanda.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Amour Hamad Amour na mkimbizi mwenge kitaifa Fredrick Ndahani (ambaye ni mwana Singida) wamezindua mkakati huo kwa kukabidhi pikipiki mbili kati ya saba kwa maafisa maendeleo ya jamii ambao ndio waratibu wa madawati hayo.
Akitoa maelezo ya Mkakati huo mara baada ya kuupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoani Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi utaufikisha Mkoa wa Singida katika azma ya kuwa na uchumi wa kati pamoja na viwanda.
Dkt Nchimbi amesema usafiri huo wa pikipiki unalenga kuwawezesha waratibu wa sekta binafsi kila halmashauri Mkoani Singida kutembelea na kutambua changamoto, fursa na mafanikio ya sekta binafsi na sio kusubiria ofisini waletewe taarifa au malalamiko.
“Dawati litatambua kwa takwimu, mahali, aina ya shughuli na hali ya uzalishaji ili kuhakikisha ushiriki mtambuka unaowajibika ipasavyo ikiwemo kutoa taarifa ya soko la mazao mbalimbali. Lengo ni kurahisisha uwekezaji mkoani kwetu”, amesema Dkt. Nchimbi.
Amesema Mkoa wa Singida unazo fursa za uwekezaji katika viwanda vidogo, vya kati na vikubwa hasa vitakavyolenga kuongeza thamani ya mazao kutokana na uzalishaji mzuri wa mazao kama ya vitunguu, alizeti na asali mkoani hapa.
Dkt Nchimbi amesema sambamba na mkakati huo mwenge wa uhuru umezindua mkakati wa kutunza mazingira wenye kauli mbiu ya ‘achia shoka kamata mzinga’ ambapo mkoa umetoa mizinga ya nyuki kwa wachoma mikaa.
Amesema mkakati huo umewalenga hasa wachoma mikaa ambao wamekiri kuwa waharibifu wa mazingira kwa kukata miti hovyo hivyo wamekubali kufuga nyuki kwa ajili ya kujitengenezea kipato cha uhakika huku wakitunza mazingira.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Amour Hamad Amour ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Singida kwa ubunifu huo unaolenga kuboresha mazingira ya kufanikisha lengo la kufikia uchumi wa kati na wa viwanda.
Amesema jitihada hizo za vitendo zinaonyesha wazi ushirikiano mzuri na kudhihirisha namna wanavyomuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano katika kufanikisha kuinua uchumi wa taifa.
Aidha amewapongeza wananchi wa Singida kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha mazao ya kutosha, amewasisitiza kuendelea kumuunga mkono Rais pamoja na kutunza umoja na amani ya Taifa.
Aidha kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Amour Hamad Amour, amefurahishwa na namna wilaya ya Manyoni ilivyokuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha dhana ya Tanzania ya viwanda inatekelezwa kwa vitendo.
Amour ametoa pongezi hizo wakati mwenge ukipita katika miradi mbalimbali wilayani Manyoni huku akiusemea mradi wa ushonaji nguo na wa ufugaji nyuki kibiashara kuwa ni ishara ya uwepo wa viwanda vidogo, vya kati na hata vikubwa siku za baadaye wilayani humo.
“Nitumie fursa hii kuwaomba maafisa wa maendeleo ya jamii, wahakikishe vikundi vya wanawake na vijana wanapatiwa mikopo kutoka asilimia tano ya mapato ya ndani ya halmashauiri ili viweze kupata nguvu ya kuanzisha viwanda vidogo. Msiishie hapo, wapeni na mafunzo mbalimbali ya ufugaji nyuki, kuku na mifugo kibiashara”, amesema Amour na kuongeza;
“Na hawa akina mama waliojiunga kwenye kikundi cha ushonaji, wapewe mafunzo ya kuboresha shughuli zao ziweze kwenda na wakati”.
Mwenge wa uhuru leo umepokelewa mkoani Singida ukitokea Mkoani Dodoma kupitia kijiji cha Sanza wilayani Manyoni, mwenge wa uhuru unakimbizwa mkoani Singida katika halmashauri saba, unakimbizwa kilomita 1064, unatembelea, kuzindua na kufungua jumla ya miradi 45 yenye thamani ya shilingi bilioni 21.9.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.