Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Cambridge Education duniani Bw. Nicholas Santcross hivi karibuni ametembea Mradi wa Shule Bora Mkoani Singida ili kujionea mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wa 2021/2022.
Akiongozana na Mshauri Kiongozi wa programu Bi Laura Mclnerney, amekutana na Kaimu Katibu Tawala Mkoa (RAS) huo Ndg Stanlous Choaji pamoja na Afisa Elimu Mkoa Dkt. Baganda Elpidius na kujadili namna ya utekelezaji wa programu unavyofanyika na bàadhi ya maboresho ili kuongeza tija katika eneo la elimu.Aidha, ugeni huo umetembelea shule za Msingi za Somoku na Nyerere ambapo walijionea madarasa yaliyojengwa kupitia Miradi ya EQUIP Tanzania na EPforR-I,utekelezaji wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) pamoja na Ushirikiano wa Wazazi na Walimu (UWaWa). Vilevile, ugeni huo ulishiriki katika upandaji wa miti kama ishara ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira shuleni kwa ajili ya upatikanaji wa kivuli na matunda.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo kutoka nchini Uingereza amepongeza jitihada za Serikali kwa kushirikiana na programu ya Shule Bora kwa namna walivyofanikiwa kuunda Ushirikiano wa Wazazi na Walimu (UWaWa) na usimamizi wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) hali iliyosababisha kuwepo kwa matokeo chanya kama vile kuongezeka kwa umahiri wa walimu katika ufundishaji, upatikanaji wa chakula shuleni, usimamizi wa elimu jumuishi, usalama wa mtoto na ushiriki wa jamii katika masuala mbalimbali ya elimu. “Nimefurahishwa na jinsi programu hii inavyotekelezwa. Ushirikiano na wadau mbalimbali wakiwemo Serikali,unaleta ufanisi katika utekelezaji wa programu hii na ni mfano wa kuigwa. Cambridge tuko tayari kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha elimu bora inapatikana”, alisema Bw. Nicholas.
Aidha, kwa upande wake RAS ameeleza kwamba programu hii imesaidia kutoa mafunzo kwa walimu yaliyokuwa na lengo la kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji ambapo tayari mafanikio yameanza kuonekana huku akieleza kufanikiwa kuongeza uhusiano baina ya Walimu na Wazazi kupitia umoja wao wa UWaWa ambapo umesaidia kuongeza idadi ya madawati, upatikanaji wa chakula shuleni na kupunguza utoro wa wanafunzi na walimu.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Mkoa wa Singida Dkt. Banganda wakati akishukuru ugeni huo ameeleza bàadhi ya mafanikio ya programu ya Shule Bora. Dr Baganda amesema kwamba programu ya Shule Bora imekuwa na tija kwani bàadhi ya mbinu za ufundishaji na usimamizi wa shule zinazotumika katika mradi wa shule Bora katika shule za msingi na Awali zimeanza pia kuigwa katika shule za Sekondari kwa kuwa zimeonekana kusaidia kuondoa mdondoko na utoro wa wanafunzi shuleni.
Hata hivyo, Dr Baganda ametaja kuwepo kwa baadhi ya changamoto ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mashine zenye uwezo mkubwa wa kuchapisha mitihani ya ndani na upungufu wa miundombinu ya shule.
Naye Samwel Daniel ambaye ni Mratibu wa Shule Bora Mkoa wa Singida alieleza kwamba ujio wa wageni hao umeongeza morali na chachu ya utendaji kazi kwa wote wanaoguswa na programu jambo ambalo amesema litaleta matokeo chanya katika utekelezaji .Aidha, Ndg Samwel ametoa wito kwa wasimamizi wa elimu katika ngazi ya Mkoa, Halmashauri, Kata na Shule kuweza kusimamia na kutekeleza kwa ufanisi shughuli zote zinazotekelezwa na Serikali kupitia Mradi wa Shule Bora ili kuboresha ujifunzaji,ufundishaji,ujumuishi na uimarishaji wa mifumo ya usimamizi wa elimu.
Shule Bora ni programu ya Serikali inayofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia UK aid. Programu hii inatekelezwa katika mikoa tisa ya Tanzania Bara kwa ushauri wa kitalamu kutoka Cambridge Education ikishirikiana na ADD International,International Resque Committee na Plan International.
Afisa Elimu Mkoa wa Singida Dkt. Banganda akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Cambridge Education duniani pamoja na baadhi ya wajumbe ambao ni waratibu wa shule bora mkoani Singida wakati alipotembelewa ofisini kwake.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Cambridge Education duniani Bw. Nicholas Santcross akishiriki upandaji miti wakati wa ziara yake mkoani Singida.
Mratibu wa Shule Bora Mkoa wa Singida Samwel Daniel ambaye akishiriki upandaji miti wakati wa ziara yake mkoani Singida.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.