Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi leo tarehe 31Julai, 2018 amewaapisha wakuu wapya wawili wa Wilaya walioteuliwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli tarehe 28 Julai, 2018.
Wakuu wa Wilaya walioapishwa leo katika viwanja vya ofisi ya mkuu wa mkoa Singida ni Bw. Pasacas Muragiri ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, Bibi. Rahabu Mwangisa Solomon ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Manyoni.
Hafla ya kuapishwa kwa wakuu hao wa Wilaya imehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe. Miraji J. Mtaturu, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi. Jackson Masaka na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe. Emmanuel Luhahula, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi mbalimbali wa Chama (CCM), Dini, Wakurugenzi wa Taasisi mbalimbali mkoa Singida, Wawekezaii pamoja na Wakuu wa Idara katika Sekretarieti ya Mkoa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amewataka wakuu wa wilaya wateule kwenda kuchapa kazi na kutatua kero za wananchi katika wilaya zao huku wakizingatia kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu.
Dkt. Nchimbi pia amewataka kusimamia ukusanyaji mapato (kodi) ya Serikali na matumizi ya fedha na rasilimali nyingine za umma sambamba na kuhakikisha vitendea kazi vipo (POS Machine), pia kuhakikisha wananchi wapo salama na pia kuhakikisha wananchi wanafanya kazi za uzalishaji mali.
"Sio vizuri kiongozi anakuja halafu wananchi wanalalamikia tunakero flani tunakero flani tunakero flani tunakero flani, inamaana sisi hatutoshi wakati sisi tupo, wakuu wa wilaya wapo, nami sitaki kuonekana sitoshi, NINATOSHA" Amesema Dkt. Nchimbi
Dkt. Nchimbi amewasihi wakuu wa wilaya kutosubiri migogoro iwafuate mezani bali kufuata wananchi pale kwenye migogoro kushughulikia haraka iwezekanavyo.
"Usisubiri migogoro ikufuate mezani, wewe toka na nenda kaiangalie hiyo migogoro ndio utakapoona na kuifahamu katika uasilia wake, jitihada kubwa ya Serikali ya awamu ya tano, ni kuhakikisha migogoro inatoweka kwa wananchi, tusiruhusu migogoro itokee kwa wananchi" amesema Dkt. Nchimbi.
Aidha amewataka wakuu wa Wilaya kusimamia miradi yote inayotekelezwa mkoani Singida na kuiorodhesha miradi yote inayotekelezwa katika wilaya zao pamoja na kuifuatilia kwa kuzingatia tarehe ya kuanza mradi, thamani ya fedha ya mradi, unatarajia kuisha lini? na hatua zake mbalimbali.
"Wakuu wa Wilaya msisubiri taarifa za maandishi, zimetuchelewesha sana, tupate taarifa za makaratasi lakini kikubwa tunataka taarifa za yanayoonekana kwa macho, tusisubiri mpaka mhusika ametuharibia" alisisitiza Dkt. Nchimbi
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.