WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harison Mwakyembe amesema sheria tarajiwa ya habari inakwenda kuleta mageuzi makubwa kwa kuipa hadhi tasnia nzima ya uandishi wa habari, ikiwemo kuifanya ianze rasmi kutambulika kama zilivyo taaluma zingine, huku akisisitiza hakuna yeyote mwenye kiwango cha elimu ya tasnia hiyo chini ya stashahada, atakayeruhusiwa kujishughulisha na uandishi wa habari baada ya 2021
Mwaka 2016 serikali ilitoa muda wa miaka mitano kwa wanahabari wote wasio na sifa ya kiwango cha elimu kuanzia ngazi ya Diploma na kuendelea kuhakikisha wanajiendeleza kufikia hatua hiyo, na kwamba ifikapo mwaka kesho ndio utakuwa ukomo wa muda stahiki
Mwakyembe aliyasema hayo kwenye kikao chake na wanachama wa chama cha Wanahabari mkoani hapa, ‘Singida Press Club’ wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua hali ya usikivu kwa wananchi kupitia Radio na Televisheni ya Taifa TBC1 na TBC Fm
“Na kuhusu suala la elimu hatutarudi nyuma, tunajua wanahabari wengi watapoteza hii kazi, ila umuhimu wa haya tunayoyachukua sasa hapo baadaye yatanyanyua sana hadhi na kuipa heshima taaluma hii…na niwahakikishie kama mtu anadhani serikali itatetereka kuhusu hili afute hiyo kichwani, ‘it’s not our concerns,’” alisema Mwakyembe
Akizungumza kuhusu tija na mageuzi yatakayotokana na uwepo wa sheria hiyo ya habari, alisema kwanza inakwenda kuanza kuitambulisha rasmi taaluma ya uandishi wa habari, sanjari na kutoa mamlaka ya kuundwa kwa bodi ya ‘ithibati’, chombo ambacho kitaainisha na kutambua nani anastahili kuwa mwana-taaluma na nani amekosa sifa kisheria
Aidha, Mwakyembe alisema, sheria hiyo inakwenda kuunda Baraza Huru la Habari, Baraza ambalo litaundwa na wanahabari wenyewe, ambao tayari watakuwa wamepitia kwenye ithibati na kuthibitika kisheria pasipo shaka kuwa hao ni wanahabari
Alisema, pia sheria hiyo inaunda Kamati ya Malalamiko, ambayo imepewa mamlaka chini ya sheria ya kimahakama ambapo jambo likiamuliwa katika kamati hiyo maamuzi yake ni sawa na maamuzi ya Hakimu wa Wilaya au Hakimu Mkazi
Hata hivyo, Waziri huyo wa Habari aliweka wazi kwamba kutokana na taaluma hiyo kuwa adhimu na kwa kuzingatia ndiyo yenye jukumu la kutoa elimu na taarifa mbalimbali kwa wananchi kupitia sheria hiyo tarajiwa kutakuwa na Mfuko wa Elimu kwa wanahabari, sambamba na kuhakikisha kila mwana-taaluma anakuwa na bima
“Tasnia hii inahitaji vijana wenye upeo mpana, waadilifu, wenye weledi na nidhamu. Na hii sheria itatufikisha huko….kwa hiyo lengo letu kubwa tukishaunda vyombo vyote hivyo tuwe na tasnia ya habari inayojiendesha yenyewe,” alisema Mwakyembe
Ili kuleta tija na ubora wa kiutendaji, na kwa kuzingatia matakwa ya kisheria ifikapo 2021, serikali imewahakikishia wanahabari kuwa itaangalia namna bora ya kujadiliana kwa pamoja juu ya uboreshaji wa maslahi na stahiki nyingine, kwa kuanzia na kiwango cha kima cha chini cha mshahara
“Pia tunakusudia kukaa chini kuaininisha na kuoanisha mitaala ya ufundishaji wa wanahabari, ili kwenda sambamba na matakwa na ubora stahiki, na sio kila mtu kuibuka na kuanzisha chuo chake cha uandishi wa habari na kufundisha anachokijua yeye hapana! hiyo haikubaliki,” alisema Waziri
Akifafanua kuhusu azma chanya kisheria kuhusu haki ya kupata habari au taarifa na huduma ya habari, alisema lengo lake ni kuzidi kuboresha ile ibara ya 18(d) katika kumsaidia mwananchi kupata taarifa kwa njia mbalimbali. Na chini ya sheria hiyo na kanuni zake kila mamlaka ina msemaji
“Badala ya kutafuta taarifa vichochoroni au kwenye vyanzo visivyo sahihi nenda kwa mtu sahihi ili akupe taarifa zisizo za upotoshaji,”
Katika hatua nyingine, akizungumzia kuhusu uchaguzi mkuu ujao, Mwakyembe alisema Serikali haitavumilia na kwamba itachukua hatua kali sana kwa chombo chochote au Mwandishi yeyote wa habari atakayejaribu kufanya upotoshaji wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi huo
Alisema kipindi cha uchaguzi ni kipindi ambacho kama watanzania tunapaswa kuonyesha mshikamano wa kitaifa, lakini kwa wanahabari suala la maadili, sanjari na kuheshimu sheria, kanuni na taratibu huku akiwataka kutumia kalamu zao vizuri ili kuepusha madhara ya uvunjifu wa amani, ambayo yanaweza kulipeleka taifa kwenye matatizo makubwa
“Na katika hili kwakweli tutakuwa wakali sana, nasubiri Tume ya Uchaguzi itawaita wanahabari wote…na safari hii naomba niwahakikishie hata watu ambao wapo kwenye mitandao ya kijamii kupitia ‘online Tv na online Radio’ kwamba na wao watafuata sheria zote za wanahabari vinginevyo tutasimamisha leseni zao,” alisema na kuongeza:
“Nawasihi sana wanahabari nyakati za uchaguzi muda ukifika tusitumike kuchafuana, tusirubuniwe na pesa na vibahasha…tuache kuandika habari kwa kigezo cha fedha tusimamie misingi na maadili.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoani hapa, Seif Takaza, kuhusu suala la kujiendeleza alimwomba Waziri kuangalia namna ya kuwasaidia wanahabari hao kupitia fungu lolote maalumu huku akisisitiza kuwa wanapenda kujiendeleza kielimu kulingana na agizo la serikali lakini kipato chao hakitoshelezi
Aidha Takaza alisema suala linalowasumbua zaidi waandishi wa mkoa huo ni kitendo cha kufanya kazi bila ya kuwa na mkataba wowote wa mwajiri, ikiwemo ule wa hali bora, huku stahiki zikiwa ni ndogo sana hali inayopelekea wao kujiingiza kwenye shughuli nyingine ili angalau kukidhi mahitaji
“Tunaamini watanzania na hata nje ya taifa letu wanampenda sana Rais John Magufuli kupitia vyombo vya habari…kwakweli asiyempenda labda ni mchawi, tunaomba serikali iangalie namna nzuri ya kuboresha na kutatua changamoto zinazotukabili ikiwepo kutupatia viwanja vya kujenga Clubs zetu kuliko kupanga kama ilivyo sasa,” alisema Takaza
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.