Serikali ya Mkoa wa Singida imekabidhi rasmi Mwenge wa Uhuru kwa Mkoa wa Tabora 26 Agosti, 2019 ambapo katika mkoa wa Singida Mwenge wa Uhuru umetembelea miradi 46 iliyohusu Sekta za Elimu, Afya, Mazingira, Maji, Utawala Bora, Kilimo, Ushirika, Biashara, na Programu za mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya, Malaria, Rushwa, Elimu ya Mpiga kura na UKIMWI. Miradi yote iliyokuwa inapitiwa na Mwenge wa Uhuru ilikuwa na thamani ya shilingi Bilioni 9,462,470,874.
Akizungumza wakati wa kukabidhi Mwenge wa Uhuru, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi, amesema miradi 12 ilikuwa inazinduliwa, miradi 2 ilikuwa inafanyiwa ufunguzi, miradi 10 ilikuwa inawekewa jiwe la msingi na miradi 22 ilikuwa inakaguliwa na kutembelewa.
Dkt. Nchimbi amesema, “Wananchi wa Mkoa wa Singida wameupokea vema ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 ambao umetolewa maeneo mbalimbali ya Wilaya za Mkoa wa Singida ambao ni: MAJI NI HAKI YA KILA MTU, TUTUNZE VYANZO VYAKE NA TUKUMBUKE KUSHIRIKI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA”.
Aidha, amesema, katika jitihada ya kuongeza huduma za Maji Mijini Mkoa wa Singida katika Miji ya Singida, Manyoni na Kiomboi imeingizwa kwenye Mradi Mkubwa wa Kitaifa utakaotekelezwa katika Miji 29 Tanzania kwa fedha za mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya India.
Amesisitiza kuwa, katika Mkopo huo Miji ya Singida, Manyoni na Kiomboi imetengewa jumla ya shilingi 87 Bilioni. Hadi hivi sasa mtaalamu mshauri aliyeingia mkataba na Serikali kwa ajili ya kuandaa nyaraka za mradi huo anaendelea na kazi.
“Kipekee kwa niaba ya Uongozi wa Serikali, Wananchi, Marafiki na Wapenzi wote wa Mwenge wa Uhuru nikupongeze Ndugu Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru na Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa kazi kubwa na iliyotukuka ambayo mmeifanya kwenye Mkoa wa Singidda na Mikoa mbalimbali kwa Umakini, Umahiri, Weledi na Uzalendo mkubwa” amesema Dkt. Nchimbi.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa mkoa wa Singida amewashukuru na kuwapongeza Vijana wote Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kimkoa, Wilaya pamoja na timu zao, viongozi, Maaskari, Madereva na Wananchi wote kwa ujumla kwa kufanikisha kazi hii.
Kwa upande wake kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2019 Ndugu Mzee Mkongea Ali, amewashukuru Watendaji wote wa Mkoa wa Singida kwa ushirikiano wa dhati walioupata wakati wote walipokuwa katika Wilaya za Mkoa wa Singida.
Pia amewapongeza kwa miradi mizuri ya maendeleo tumeona kwa namna gani mnavyopaambana na adui ujinga tumeona viwango vizuri vya shule, tumeona kwa namna gani ambavyo mnapambana na adui maladhi tumeona vituo vya afya vyenye viwango ya hali ya juu, tumeona kwa namna gani mnavyopambana na adui maskini tumeona kwa namna gani asilimia 10 inavyomfikia mlengwa" Amesema Ndugu Mzee Ali Mkongea.
Akihutubia kwa nafasi mbalimbali, Ndugu Mzee Mkongea, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, ametoa wito kwa Wananchi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kwenda kupiga kura kwa amani na usalama, kujitokeza kwenye mikutano ya kampeni ili kwenda kusikiliza sera, ili kuweza kumpima kiongozi kama anafaa au hafai.
"Hivyo nichukue fulsa hii, kuwasihi kwenda kuchagua viongozi bora waadilifu, waaminifu ambao wana kariba kama ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli." Amesema Mkongea.
Imetolewa na;
Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
SINGIDA
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.