Katibu Tawala Mkoa wa Singida Mwl. Dorothy Mwaluko ametoa muda wa siku saba (wiki moja ) kwa Afisa Elimu Kata, Mtendaji na kamati za shule kuhakikisha vyumba vyote vya madarasa katika Shule ya Msingi Kilimatinde iliyopo kata ya Kilimatinde Wilaya ya Manyoni vinawekwa sakafu.
Maelekezo hayo ameyatoa leo baada ya uwekaji wa jiwe la msingi katika jengo la ofisi ya Afisa Tarafa wa Tarafa husika ambapo pamoja na mambo mengine alitaka kupata taarifa ya shule hiyo ya msingi ikiwemo uwepo wa vyoo, madarasa na madawati.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Mwl. Dorothy Mwaluko (kulia) akisisitiza jambo kwa Afisa Elimu wa Kata hiyo Laura Athanas wakati wa ziara hiyo Wilayani Manyoni.
Mwaluko alisema kwamba ni Mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba kila shule inapata ruzuku ya elimu bure (Capitation grant ) ambapo alifafanua kwamba Mwalimu Mkuu pamoja na Afisa elimu wangeweza kuilekeza katika ujenzi wa sakafu hizo na kuwaondolea wanafunzi changamoto ya kusoma kwenye madarasa yenye vumbi.
"Mnapopata capitation msikimbilie kununua chaki angalieni namna itakavyowezekana ndani ya siku saba vyumba hivyo viwe vimewekewa sakafu, Afisa Elimu na Mtendaji shirikianeni muwashawishi wazazi na mafundi wajitolee nguvu kazi hiyo ikamilike" alisema.
Hata hivyo Afisa Elimu wa Kata hiyo Laura Athanas, alieleza kwamba katika shule hiyo wana jumla ya wanafunzi Mia nne (400) hivyo kupata ruzuku ndogo ikilinganishwa na shule nyinge jambo ambalo RAS alikataa vikali kwa mifano kwamba zipo shule zinapata fedha kidogo lakini bado wanaweza kufanya na kusimamia mipango ikakaa vizuri.
Aidha, RAS huyo alianzisha harambee ya kuchangia mifuko ya saruji ambapo alitoa mifuko mitano, Afisa Elimu naye akatoa mifuko miwili, huku Menejimenti ya Mkoa huo ilitoa jumla ya mifuko 10 kwa ajili ya uwekaji wa sakafu katika vyumba hivyo.
Ziara hiyo ilihusisha Menejiment ya Mkoa huo na walitembelea Ujenzi wa nyumba ya Afisa Tarafa kata ya Nkonko na Kilimatinde pamoja na ukaguzi wa Ujenzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana Solya na Hospitali ya Wilaya ya Manyoni.
MATUKIO KATIKA PICHA
Ukaguzi wa Ujenzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana Solya Wilayani Manyoni.
Ukaguzi Hospitali ya Wilaya ya Manyoni
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.