Serikali mkoani Singida, imewataka wananchi kuwa na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ili kubaini magonjwa ambayo yanachukua muda mrefu kujitokeza, na kuacha tabia ya mtu kusubili hadi afya iwe na mgogoro ndipo akapime.
Agizo hilo limetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi, wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kampeni ya mapambano dhidi ya Saratani mkoani Singida.
Dkt. Lutambi amesema, ugonjwa wa Saratani ukibainika katika hatua zake za awali, upo uwezekano wa kutibika endapo mgonjwa atazingatia kikamilifu ushauri wa wataalamu.
“Ni vema kila mmoja wetu kuwa na desturi ya kupima afya mara kwa mara ili kutambua hali ya kiafya. Endapo utatambulika una ugonjwa wa Saratani, hakikisha unapata huduma za afya kulingana na ushauri utakaopewa na wataalamu wa Afya”.
Amesema, wale waliokwisha jitambua kuwa na saratani, waendelee kutumia huduma za afya ili kuepuka athari zitokanazo na ugonjwa huo hatari wa saratani.
Akitaja baadhi ya vyanzo vya ugonjwa wa saratani, Dkt. Lutambi amesema, vyanzo vikubwa vya saratani ni pamoja na matumizi ya tumbaku na bidhaa za ugoro.
“Matumizi ya tumbaku ni kisababishi kikubwa cha magonjwa ya Saratani ya Matiti, mdomo, koo pamoja na ugonjwa wa moyo. Pia unywaji wa pombe uliopitiliza kusababisha magonjwa ya Saratani ya Matiti, Ini, Utumbo mpana, pamoja na saratani nyingine.
Aidha, amewataka wananchi kujiepusha na visababishi vya ugonjwa huo wa Saratani kwa kuwa ni ugonjwa hatari kwa maisha ya binadamu.
Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Singida, kwaniaba ya wananchi wa mkoa wa Singida, ameishukuru taasisi ya Saratani ya hospitali ya Ocean Road ya jijini Dar es salaam kwa kutuma madaktari kuja kutoa huduma za kitabibu kwa wakazi wa mkoa wa Singida.
Awali, Meneja kitengo cha uchunguzi wa Saratani hospitali ya Ocean Road, Dk. Maguha Stephano, amesema pamoja na kutoa huduma ya afya, pia wametoa mafunzo ya awali juu ya kutambua saratani kwa baadhi ya wataalamu wa afya mkoa wa Singida, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kutambua saratani.
“Taasisi yetu ya Ocean Road inatembea kwa maono ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya TANO, Dkt John Magufuli na ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo ni Watanzania kuwa na afya njema”. Dk. Maguha Stephano.
Wakati huo huo mkazi wa Mtaa wa Munugh’una Manispaa ya Singida, Bi. Mwanaidi Kipandwa, ameishukuru taasisi ya Ocean Road, kwa uamuzi wake wa kusogeza karibu huduma ya utabibu kwa kuitoa bure kwa wakazi wa mkoa wa Singida.
“Wengi wetu hapa tulipo kufika Dar es salaam ni mtihani mkubwa. Naiomba taasisi ya Ocean Road isichoke, ijenge utaratibu wa kuleta au kusongeza huduma hii muhimu sana kwetu sisi tusio na uwezo wa kufuata huduma za matibabu Dar es salaam”, Amesema Bi. Mwanaidi Kipandwa.
Kampeni hii inatekelezwa kwa siku tano mkoani Singida na timu ya wataalamu kutoka hospitali ya Ocean Road ya jijini Dar es salaam.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.