Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Halima Dendego, amefungua mkutano wa kimataifa wa kongamano la wanawake kanda ya Afrika Mashariki na Kati katika Kanisa la Waadventista Wasabato Ititi, mkoani Singida.
Katika mkutano huu, waumini takribani 3000 kutoka Mataifa mbalimbali ikiwemo Uganda, Congo, Somalia, Djibouti, Eritrea, Sudan Kusini, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Kenya na wenyeji Tanzania, wamekusanyika ili kujadili masuala muhimu yanayohusu wanawake katika maeneo yao hususan ustawi wa jamii.
RC. Dendego ametoa shukrani za dhati kwa washiriki kwa kuchagua Nchi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa kongamano hilo la kimataifa akisema maamuzi hayo ni sahihi kwa kuwa Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwa nchi yenye amani, ukarimu, na utulivu, hali ambayo imerahisisha kufanyika kwa mkutano huu muhimu.
Aidha, Mkutano huo umeelekezwa katika kuwasaidia wanawake kutambua uwezo wao katika kumtumikia Mungu na kusaidia jamii zao huku akikiri mchango wa wanawake katika jamii, akisema wanao uwezo mkubwa waliopewa na Mungu.
Amesisitiza umuhimu wa wanawake kujiamini na kuzitambua fursa zilizopo ili waweze kuchangia maendeleo ya jamii na taifa. Pia ametoa wito kwa wanawake kuondokana na dhana ya kutegemea kuwezeshwa na badala yake wajitambue kama nguvu kazi muhimu katika jamii akisema hakuna mafanikio katika jamii wala kwa mwanaume bila uwepo wa mwanamke imara.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Dendego alikumbusha wanawake wajitahidi kutimiza majukumu yao ya kuwa wazazi na walezi kwa kuhakikisha maadili mema kwa watoto wa kike na wa kiume. Aliweka wazi athari za kumomonyoka kwa maadili na kuibuka kwa vitendo vya kinyume na mila, desturi, na imani za kidini, akisisitiza umuhimu wa kupinga vitendo vya mahusiano ya jinsia moja na usafirishaji haramu wa binadamu.
Kama sehemu ya hafla hii, Mheshimiwa Dendego amewahakikishia washiriki usalama wakati wote watakapokuwa Singida na kuwakaribisha katika Maonesho ya kitaifa ya Mifuko na Programu za uwezeshaji yanayofanyika katika viwanja vya Bombadia, Singida mjini.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewahamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.