Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, amepiga marufuku Wananchi wa Mkoa huo kuanza kunywa pombe wakati wa kazi (asubuhi) na kuwataka kutumia muda huo kufanya shughuli za maendeleo ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kujenga uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Dendego, ametoa kauli hiyo leo (19 Aprili, 2024) katika Kijiji cha Kashangu, Halmashauri ya Itigi kwenye ziara yake ya kikazi ya Siku Mbili kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya Elimu na Afya.
Aidha ameonya kuwa hatasita kuwachukulia hatua Viongozi wa Vijiji na Kata ambao watashindwa kudhibiti hali hiyo ya unywaji wa pombe nyakati za asubuhi badala ya kuhimiza wananchi kwenda kufanya shughuli halali za kijitafutia riziki.
“Mnaanza kunywa Pombe asubuhi hasa watoto wa kike hii Sio sawa lazima tusimamiane nikikuta jambo linaenda ndivyo sivyo nitakamata Mtendaji kwa sababu anasheria kama zangu na kwanini ashindwe kudhibiti vitendo hivyo tutawajibishana vikali,” Amesisitiza RC Halima Dendego.
Kuhusu utoaji wa chakula mashuleni, amewaagiza Wakuu wa Shule zote za Mkoa wa Singida kwa ushirikiano na Viongozi wa Vijiji na Kata kuweka utaratibu wa kutoa chakula kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanajifunza kwa bidii.
Amesema utoaji wa chakula mashuleni utasaidia kwa kiasi kikubwa kupandisha ufauli kwa wanafunzi hivyo ni muhimu kwa kila shule kuanza utaratibu wa kutoa chakula kwa wanafunzi wao.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga amewataka Watendaji wa Halmashauri na Kata Mkoani humo kusimamia vizuri ujenzi wa miradi ya maendeleo hasa umaliziaji wa majengo mbalimbali ili kudhibiti vitendo vya wizi wa vifaa vya ujenzi.
Amesema hatapenda kusikia wala kuona wizi wa vifaa katika miradi ya maendeleo hivyo Viongozi lazima wasimamie kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na ubora ambao utaleta manufaa kwa Wananchi na sio vinginevyo.
Katibu Tawala huyo wa Mkoa amesema kumekuwa na tabia ya kuiba vifaa hasa vinapopelekwa kwenye miradi ya maendeleo jambo ambalo linasababisha utekelezaji wa baadhi ya miradi kujengwa chini ya kiwango na kusisitiza kuwa tabia hiyo itakoma iwapo Viongozi wote watashirikiana katika ngazi zote.
Ziara hiyo ya Siku mbili ya Mkuu wa Mkoa huo itaendelea kesho (tarehe 20 Aprili, 2024) ambapo atakagua Ujenzi wa nyumba ya Walimu katika Shule ya Sekondari Kitaraka, Kihanju kukagua Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya pamoja na kusikiliza na kuzitatua kero za wananchi wa Halmashauri hiyo ya Itigi mkutano utakaofanyika katika ofisi ya kijiji cha Songambele.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.