MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ameanza ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Mkalama na kutoa agizo kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuhakikisha ifikapo Juni 20, mwaka huu iwe imekamilika.
Pia ametoa agizo baadhi ya miradi kama ya ujenzi wa shule mpya za msingi ujenzi uwe unafanyika kwa saa 24 na kuongeza idadi ya mafundi ili kuongeza kasi ya ujenzi na kumwagiza Meneja wa Shirika la Umeme (TANESCO) Wilaya ya Mkalama kupeleka umeme kwenye miradi hiyo ili kuwezesha mafundi kufanya kazi muda wote.
Ametoa agizo hilo leo (Mei 26, 2023) katika siku ya kwanza ya ziara yake Wilayani Mkalama ambapo alitembelea na kukagua miradi sita ambayo ni ujenzi wa shule mpya za msingi, ujenzi wa mabweni, vyumba vya madarasa, vyoo, zahanati na Hospitali ya Wilaya ya Mkalama.
Serukamba alianza kwa kutembelea kikundi cha watu wenye ulemavu Iguguno kinachojishughulisha na biashara ndogondogo, ukamlilishaji wa ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Lukomo na ujenzi wa shule mpya ya msingi Ishenga.
Akiwa katika mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Ishenga alimwagiza Mhandisi wa Wilaya kuhakikisha kila siku awe anafika kwenye mradi huo kukagua kuona ujenzi unavyoendelea na atembelee kila jengo kujua changamoto iliyopo kwa mafundi na kuitatua.
“Mhandisi wa Wilaya kwanza wewe ubaki hapa hapa kwenye mradi hakuna haja ya kuendelea na mimi kwenye ziara baki usimamie tunataka mradi huu ifikapo Juni 7, mwaka huu ujenzi wa shule hii uwe umekamilika,” alisema Serukamba.
Katika mradi wa ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuari ya Wilaya ya Mkalama ambayo Serikali imeshatoa Sh. Milioni 300, aliagiza ifikapo Juni 20, mwaka huu ujenzi uwe umekamilika na kukabidhiwa kwa Serikali.
Mkuu wa Mkoa akiwa katika mradi wa ujenzi wa matundu ya vyoo 17 shule ya msingi Mazilinga alimwagiza Afisa Elimu Shule za Msingi kuhakikisha anasimamia kwa karibu ujenzi huo na uwe umakalimika ifikapo Juni 19, mwaka huu.
Aidha, Serukamba alitoa agizo la jumla kwa Mhandisi wa Ujenzi wa Mkoa katika shule tisa mpya za msingi zinazojengwa kwenye Halmashauri kutokana na fedha za mradi wa BOOST kuanzia Jumatatu wiki ijayo aanze kuitembelea na kuangalia maendeleo ya ujenzi na siku ya Ijumaa ampelekee ripoti.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.