Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Idara wametakiwa kutumia Saikolojia kubwa katika usimamizi na utawala wa watumishi ambao wameonekana kuchelewesha utekelezaji wa majukumu yao ili kutatua changamoto za makusanyo na uzalishaji au ucheleweshaji wa ufungaji wa hoja za ukaguzi (CAG) zilizopo katika maeneo yao.
Maelekezo hayo yametolewa leo tarehe 20.06.2023 na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, wakati wa Mkutano maalum wa kupitia hoja za ukaguzi uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika shule ya Sekondari ya Ilongero.
Serukamba ametoa maelezo hayo baada ya kubainika kwamba Afisa Ugavi wa Halmashauri ya Wilaya Singida hakuwa ametekeleza majukumu yake ipasavyo hasa katika kusimamia na kutoa nyaraka muhimu za manunuzi ambazo zingesaidia kufunga hoja za ukaguzi pamoja na kwamba alitakiwa kufanya hivyo katika vikao mbalimbali vilivyopita.
Kutokana na hali hiyo viongozi mbalimbali walilalamikia utendaji kazi wa Afisa Ugavi huyo swala ambalo lilimlazimu RC Serukamba kutoa somo juu ya kushughulika na watu wa namna hiyo ili kazi za Serikali ziendelee wakati ikitafutwa njia mbadala.
Alisema inawezekana kuna watumishi ambao hawawezi kutimiza majukumu yao mpaka wafuatiliwe kwa ukaribu na baadhi ya wengine wanachangamoto nyingi za kifamilia hivyo ni vyema saikolojia itumike katika kusimamia utendaji kazi wa watu hao.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga, amewataka kutembelea Chuo cha Uhasibu cha Mkoani Singida na kuomba wanafunzi wa mazoezi wa gani za ugavi ili kumuongezea nguvu Afisa huyo.
Alisema wakati Serikali inajipanga kuajiri watumishi wapya katika Halmashauri hiyo inaweza kupokea wataalamu wa kujitolea na kuwalipa fedha za kujikimu kupitia mapato ya ndani ili kuepuka kuzalisha hoja katika upande wa manunuzi.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Ester Chaula, ameeleza kwamba pamoja na changamoto ambazo zipo bado wanajitahidi kabla ya kufikia tarehe 30 June, hoja hizo zimefungwa zibaki zile za kisera ambazo zipo nje ya uwezo wao.
Hata hivyo aliendelea kusema kwamba Halmashauri hiyo ilikuwa na hoja 68 lakini zilizofanyiwa kazi ni hoja 36 jambo ambalo waliahidi kuendelea kuzipunguza zaidi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Singida Ester Chaula, akizungumza wakati wa Mkutano huo.
Mkuu wa Wilaya ya Singida DC Mhandisi Paskas Muragili akizungumza wakati wa Mkutano huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Singida Vijijini Eliya Digha, akifunga mkutano huo.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.