MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote Mkoani hapa kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa vyumba 290 vya madarasa kabla ya Disemba 15 mwaka huu.
Alisema kukamilisha ujenzi huo mapema kutawezesha wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwakani kuanza masomo bila usumbufu wowote.
Ametoa agizo hilo leo Novemba 4, 2022 baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Manispaa ya Singida, Halmashauri za Wilaya ya Ikungi na Manyoni.
"Kama tulivyokubaliana ujenzi wa madarasa yote 290 ambayo Serikali imetoa fedha Sh.bilioni 5.8 katika Mkoa wetu uwe umekamilika kabla ya Disemba 15, mwaka huu," alisema.
Serukamba akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa sita katika shule ya Sekondari ya Mughanga Manispaa ya Singida, alimwagiza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa, Jeshi Lupembe kuunda kamati ambayo itakuwa inapita kila siku jioni kuangalia maendeleo ya ujenzi wa madarasa.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alielekeza fedha zitakazokuwa zimebaki wakati wa ujenzi huo utakakuwa umekamilika zielekezwe kununua madawati.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Jeshi alimhakikisha Mkuu wa Mkoa kuwa ujenzi wa madarasa 50 ambayo Manispaa imepewa na Serikali Sh.bilioni 1 utakamilika Novemba 30, mwaka huu.
Jeshi alisema ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Manispaa hiyo upo katika hali nzuri isipokuwa katika shule za Sekondari za Unyanga na Mfumu ambako mchakato wa kuzihamisha fedha ulichelewa lakini suala hilo limeshapatiwa ufumbuzi na kazi ya ujenzi imeshaanza.
Akiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi alitembelea ujenzi wa madarasa katika shule za Sekondari za Ikungi na Unyahati.
Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi, Justice Kijazi, alisema Serikali imetoa Sh.milioni 580 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 29 katika Halmashauri hiyo.
Alisema ujenzi wa madarasa 20 yapo hatua nzuri za ujenzi na kwamba kabla ya Disemba 15 yote yatakuwa yamekamilika.
MWISHO
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.