MKUU wa Mkoa Singida, Peter Serukamba, amewagiza watendaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kuhakikisha wanaosimamia miradi inayotekelezwa wilayani humo ikamilike yote kabla ya Juni 30 mwaka huu.
Aidha, ametoa agizo kwa miradi ya ujenzi wa shule mpya za msingi inayojengwa kwa fedha za BOOST Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lipeleke huduma ya umeme maeneo ya mradi ili kazi ya ujenzi ifanyike usiku na mchana.
Serukamba ametoa agizo hilo baada ya kufanya ziara ya siku mbili kukagua miradi ya ujenzi wa shule mpya za msingi, zahanati, vituo vya afya, mabweni, madarasa na vyoo ambayo Serikali imetoa mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuitekeleza.
"Tunaipongeza sana Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeleta fedha nyingi sana kwenye Halmashauri hivyo ambao tumepewa nafasi ya kuwa viongozi kazi yetu ni kuhakikisha fedha hizo zinafanya kazi iliyokusudiwa miradi ikamilike kwa wakati na izingatie 'value for money'," alisema.
Mkuu wa Mkoa alisema moja ya maelekezo mahsusi yaliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah Kairuki, ni kuhakikisha kusiwe na bakaa yaani fedha zinarudi baada ya mwaka mpya wa fedha kwisha badala yake miradi yote inakwisha.
"Mkalama kwenye shule zinazojengwa kwa fedha za BOOST kasi sio nzuri sana ndio maana nimempa maelekezo Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ahakikishe kila siku anatembelea miradi na kutoa maelekezo kwa mafundi ili miradi ikamilike Juni 20 mwaka huu," alisema.
Serukamba alisema kuanzia sasa kazi ya ujenzi wa miradi hiyo iwe inafanyika hata siku za Jumamosi ili kukimbizana na muda kwani asingependa kuona baada ya Juni 30 fedha zinarudishwa serikalini kwasababu miradi haijakamilika.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mkalama, James Mkwega, alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kwamba miradi yote katika Wilaya hiyo itamalizika kwa muda uliipangwa.
Mwisho
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.