MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, leo (Juni 14, 2023) amezindua Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji utakaogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 34. 176 utakaotekelezwa katika Kijiji cha Msingi, Kata ya Msingi Wilayani Mkalama mkoani Singida.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi huo ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18, alisema Mradi wa Skimu ya Msingi utakuwa na jumla ya eneo la hekta 2,000.
Serukamba alisema mradi huu utakapokamilika utawanufaisha wakazi 12,000 kutoka Vijiji vinne vya Ishinsi, Ndurumo, Msingi na Kidi vilivyopo Kata ya Msingi Tarafa ya Kinyangiri ambao watalima mazao ya mpunga, mahindi na mbogamboga kwa misimu miwili hadi mitatu kwa mwaka.
Alisema shughuli kuu zitakazofanyika katika shughuli ya ujenzi wa mradi ni ujenzi wa bwawa lenye ujazo wa Lita 1,875,000, ujenzi wa mifereji ya umwagiliaji yenye kilometa 19.12, uchimbaji wa mifereji ya matupio yenye urefu wa kilo mita 42.539, uchimbaji wa mifereji ya kuingiza maji mashambani yenye urefu wa jumla ya kilometa 34.778.
Shughuli nyingine zitakazofanyika ni ujenzi wa barabara za mashamba zenye urefu wa kilomita 36.1, kusawazisha ekari 2,000 za mashamba, ujenzi wa kilomita nane za barabara na makaravati sita kuelekea ndani ya mradi na ujenzi wa vigawa maji 14, vipunguza mwendo, viumbo angalizi 90, vipitisha maji 90, makaravati 14 pamoja na vivuko nane.
Mkuu wa Mkoa alisema ili Mkandarasi aweze kuendelea na kazi za ujenzi bila kukwama Tume ya Umwagiliaji ihakikishe inamlipa Mkandarasi kila anapokamilisha hatua mojawapo ya ujenzi.
Akizungumza na wananchi wa vijiji vitakavyonufaika na mradi huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la mradi, Mkuu wa Mkoa huyo aliwataka wananchi kutouza ardhi kwani lengo la Serikali ni kutaka wenyeji wafaidike na mradi huo.
Serukamba aliwaondoa hofu wananchi kwamba watanyang'anywa ardhi kwamba hizo ni propaganda hakuna atakayenyang'anywa na kuagiza wenyeviti wa vijiji kusimamia kuhakikisha kila mwananchi anapata eneo la kulima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymondi Mndolwa, alisema pamoja na kwamba sio jukumu la Tume hiyo kujenga barabara lakini katika mradi huo zimetengwa fedha kwa ajili ya kujenga kilometa nane ili kuwawezesha wananchi kupata urahisi wa kusafirisha mazao yao kutoka mashambani.
Alisema katika mwaka wa fedha ujao Tume hiyo itajenga ghala la kuhifadhia mazao katika kata hiyo ya Msingi ili wakulima wakishavuna wanayahifadhi kwa ajili ya kusubiri kuyauza na kwamba ni jukumu la viongozi wa kijiji kutenga eneo litakapojengwa ghala hilo.
Mndolwa alisema wakati Serikali inajenga miundombinu hiyo ya umwagiliaji wakulima wana wajibu wa kulipa ada ya umwagiliaji fedha ambazo zitakuwa zinawekwa kwenye akaunti maalum ambazo zitatumika kwa ajili ya ukarabati na uendelezaji wa sehemu nyingine zenye miradi hapa nchini.
“Wakati mnaushangilia mradi huu mjue kwamba mtakuwa na miundombinu mizuri mkilima vizuri lakini mtapaswa kulipa ada ya umwagiliaji, msipolipa nitafunga bomba na nitalifunga bomba sio kwa macho hautaniona nitafunga kwa mtandao kwa hiyo huna pa kunikamatia,” alisema.
Aidha, Mkurugenzi huyo aliwataka wananchi wa kata hiyo kumsimamia Mkandarasi aliyepewa zabuni ya kujenga miundombinu ya umwagiliaji ili akamilishe mradi huo kwa wakati lakini pia kuhakikisha hawamwibii vifaa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali, alimshukru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha za ujenzi wa mradi huu na kwani utasaidia kuinua uchumi wa Wilaya hiyo.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, James Mkwega, alisema fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika mradi huu ni nyingi hivyo watahakikisha wanautunza ilu wanufaike na kubadili maisha ya Wananchi.
MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Pancras Steve akitoa utambulisho wa viongozi mbalimbali walioambatana na Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi, Paskas Muragili akitoa akizungumza kwa niaba ya wakuu wa Wilaya wa mkoa wakati wa hafla ya makabidhiano ya mradi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, akizungumza na wananchi wa vijiji vitakavyonufaika na mradi huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la mradi
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymondi Mndolwa, akizungumza na wananchi wa vijiji vitakavyonufaika na mradi huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la mradi.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kushuhudia makabiadhiano ya mradi huo.
Picha ya pamoja mara baada ya makabidhiano ya mradi.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.