Mkuu wa mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, amepiga marufuku madereva wa bajaji na pikipiki katika Manispaa ya Singida kulipa tozo yoyote bila kupewa risiti na mtu anayetoza tozo hizo kwakuwa ni kinyume na utaratibu wa Serikali.
Dendego, ametoa kauli hiyo (leo Aprili 25, 2024) kwenye Mkutano wake na Madereva wa Bodaboda na Bajaji katika Viwanja vya Bombadia kwa ajili ya kusikiliza kero zinazowakabili madereva hao na kuzitafutia ufumbuzi.
Amesema ni jambo la aibu kwa Watendaji wanaokusanya mapato ya Serikali na kutotoa risiti wakati msisitizo mkubwa wa Serikali ni kuwa malipo ya aina yoyote lazima mnunuzi apewe risiti halali ili Serikali ipate mapato kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Haiwezekani kwa Serikali tuwe wa kwanza kutotoa risiti hilo halipo na haitawezekana tunataka haki bini haki, Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida ukakae na Mzabuni ili muweke utaribu wa kutoa risiti kama Serikali inavyoelekeza”. RC Dendego
Kuhusu mikopo ya Halmashauri, Mkuu huyo wa mkoa wa Singida amemwagiza Mkurugenzi wa Manispaa kukaa na Viongozi wa Madereva Pikipiki na Bajaji wa Halmashauri ya Manispaa hiyo ili awasaidie kuanzisha chama cha kuweka na kukopa – SACCOS - chama ambacho kitawasaidia kukopa fedha kwa ajili ya kununua vyombo vyao vya usafiri badala ya kuendesha vya watu hali ambayo itawasaidia kuboresha maisha yao.
Amesema kwa sasa chama chao kina wanachama zaidi ya 4,000 hivyo wanaweza kukopeshwa na kurejesha mikopo yao kwa haraka kama Watendaji watawasaidia kuanzisha SACCOS yao.
“Wakianzisha SACCOS yao wapelekeeni milioni 200 waweze kukopeshana wao kwa wao kwa sababu wanajua na ulipaji wao utakuwa ni rahisi kuliko kukopesha makundi mengine ambayo hayaeleweki kwani watajiimarisha kiuchumi kwa kununua vyombo vyao vya usafiri kwa sababu kazi wanaiweza” amesisitiza RC Dendego.
Naye, Mwenyekiti wa Madereva wa Bodaboda na Bajaji Manispaa ya Singida Abdi Mitigo, amemshukuru Mkuu wa mkoa wa Singida kwa kukutana nao na kutatua kero mbalimbali ambazo zilikuwa zinawanyima usingizi na kushindwa kufanya kazi ikiwemo tozo na ushuru hivyo amesema kwa sasa watachapa kazi kwa raha bila usumbufu.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.