MKUU wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, amejinasibu kuwa Mkoa wake kwa sasa unaendelea vizuri katika suala la kuwa na kilimo bora na cha kisasa na kusababisha kuwa na ziada ya chakula cha kutosha.
Serukamba ametoa kauli hiyo leo tarehe 2 Agosti, 2023 wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yaliyofanyika kikanda katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.
Mkuu huyo wa Mkoa, amesema kuwa mkoa huo unategemea zaidi pato linalotokana na kilimo, mifugo na uvuvi na kueleza kuwa kutokana na hali hiyo maonesho hayo yatakuwa chachu katika kusukuma maendeleo kwa kutumia teknolojia zitakazooneshwa.
Alisema kuwa shughuli za kilimo zinaendelea kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kujihakikishia usalama wa chakula na malighafi ya kulisha viwanda vilivyopo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutembelea mabanda katika sherehe za ufunguzi wa Maonyesho ya Wakulima, Wafugani na Wavuvi yaliyofanyika kikanda katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.
Aidha amesema kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka Tani 477,967 mwaka 2016/17 hadi kufikia Tani 726/771.3 mwaka 2021/2022 na kuwa na ziada ya Tani 184,595.6 kutokana na makadirio ya idadi ya watu 2,008,058 waliopo katika mkoa.
Mbali na hilo alisema kuwa uzalishaji wa mazao ya biashara umeongezeka kutoka Tani 151,965 mwaka 2016/17 hadi kufikia Tani 342,405.5 mwaka 2021/22.
Alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2023/24 Serikali imeupatia Mkoa wa Singida kiasi cha sh.bilioni 34.17 kwa ajili ya ujenzi wa Skimu ya umwagiliaji ya msingi iliyopo Wilaya ya Mkalama yenye jumla ya Ekari 2,000 na sh.bilioni 1.8 kwa ajili ya kuanza shughuli za awali za ujenzi wa skimu ya Tyame, Masagi iliyopo Wilaya ya Iramba yenye jumla ya Ekari 4000.
Amesema kuwa miradi mingine itakayo anza kutekelezwa katika mwaka 2023/24 katika Mkoa wa Singida ni pamoja skimu 15 zenye jumla ya ekari 13,833 zitafanyiwa upembuzi yakinifu, usanifu na ujenzi skimu 12 zenye jumla ya ekari 7285 zitakazofanyiwa upembuzi na ukarabati, mabwawa 6 yatafanyiwa upembuzi yakinifu usanifu na ujenzi ambayo yatamwagilia eneo lenye jumla ekta 4900.
“Tunaratajia kuwa baada ya kukamilika baada ya utekelezaji wa miradi Mkoa utakuwa na eneo lenye jumla ya ekta 32,018 za umwagiliaji sawa na asilimia 65.85 zenye eneo lote la ekta 47,000 zinazofaa kwa umwagiliaji zilizopo na wakulima 80,045 watakao nufaika.
“Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na wadau wa kilimo na ufugaji, utaendelea kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji juu ya matumizi ya kanuni bora za kilimo na ufugaji”.
“Matumizi ya pembejeo za kilimo na ufugaji yanasisitizwa ili kuhakikisha kuwa tija ya uzalishaji inaongezeka, katika kipindi cha mwaka 2022 /23 kiasi cha tani 395.38 za mbegu za alizeti ruzuku ya Serikali ya sh.bilion 3.1 zilizopelekwa na kutumika na wakulima.
“Aidha mbolea yenye ruzuku ya Serikali kiasi cha tani 2973 zenye thamani ya sh.bilioni 4.1 zilizopokelewa na kutumika na wakulima, katika sekta ya mifugo jumla ya lita 2664 za madawa ya kuogesha mifugo zenye thamani ya shilingi 119,880,000 zilizopokelewa na kutumika na wafugaji” ameeleza Serukamba.
Akiendelea kutoa taarifa ya Mkoa wa Singida Serukamba alisema kuwa jumla ya Majosho 34 yamejengwa kwa gharama ya sh. 742,000,000 na kueleza kuwa Mkoa utaendelea ushirikiana na wadau ili kuhakikisha pembejeo za kutosha zinapatikana na kuwafikia wanufaika kwa muda muafaka ili kuhakikisha kuwa tija ya uzalishaji inaongezeka katika sekta za kilimo na mifugo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, wakati wa kufungua maonesho hayo amesema kuwa maonesho yamelenge kuwapatia elimu wakulima, wafugaji na wavuvi kwa lengo la kuwanufaisha katika kuendesha ufugaji na kilimo chenye tija zaidi.
Hata hivyo Senyamule alisema kuwa maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati yamekuwa na ubunifu mkubwa kwa maana ya kuwa na makongamano ya kutoa elimu juu ya kilimo cha Alizeti, Mtama na Kuku kwa lengo la kuwapatia elimu wakulima ili kuweza kuwa na kilimo chenye tija badala ya kuendesha kilimo cha kujikimu.
Hata hivyo amewataka wadau wote wa kilimo kuhakikisha wanashiriki kwa uaminifu kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali ambayo yatawafanya kujiongezea kipato wao, jamii na taifa kwa ujumla wakati wa utekelezaji wa shughuli zao za masuala yanayohusu kilimo, ufugaji na uvuvi.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.