MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amezipongeza Halmashauri zote za mkoa wa Singida kwa kupata hati safi, kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Dkt. Nchimbi, ametoa pongezi hizo wakati akizungumza katika kikao Maalum cha Baraza la Madiwani cha hoja za ukaguzi kilichofanyika katika ukumbi wa zamani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Amesema, Watumishi na Watendaji ni waajiriwa wa Serikali iliyoko madarakani, ni lazima wawe waaminifu na waadilifu kwani ndiyo inayowalipa mshahara.
‘’Ukiona mahali kuna hoja za ukaguzi, ujue kiwanda cha kuzalisha hoja ni watumishi na watendaji, sisi watumishi na watendaji tukikaa vizuri hakutakuwa na hoja, ninyi ambao hamkuwepo wakati hoja za ukaguzi zilipokuwa zinazalishwa na watendaji waliopita onyesheni mfano basi msiwe na dhana ya kukariri, kunakilishwa halafu ninyi wenyewe hamuonyeshi mabadiliko, hivyo inawapasa kuonyesha kwamba sisi hatuna hoja ndipo hapo tutakapokutana na kujipongeza kwamba tumepata hati safi’’ Dkt. Nchimbi
Amesema, ni lazima watumishi na watendaji wazingatie hasa kwa utumishi wa awamu ya tano, awamu ambayo si ya maslahi binafsi bali ni ya kutekeleza agenda za kitaifa.
‘’Sisi sote ni wasaidizi wa Mheshimiwa. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais ambaye hafanyi kazi kwa maslahi yake, hivyo inawapasa kuwa makini sana katika utendaji wenu”. Amesisitiza Dkt. Nchimbi
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida amezipongeza kwa dhati Halmashauri zote za Mkoa wa Singida kwa kupata hati na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika kuwatumikia Wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi, amesema kuwa kuna hoja zingine hazikuwa za lazima bali ni uzembe wa watendaji ambao hawakuwa makini katika kutekeleza majukumu yao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba Bw. Linno Mwageni, aliwasilisha hoja za ukaguzi 64 na kutoa taarifa ya Halmashauri hiyo kupata hati safi kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
IMETOLEWA NA,
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
OFISI YA MKUU WA MKOA
SINGIDA
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.