Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge leo ametembelea masoko ya Kilambida, Mitunduruni na Mahembe yaliyopo katika Manispaa hiyo lengo likiwa ni kukagua mazingira ya usafi pamoja na maeneo waliyokwisha pangiwa kufanyia biashara ya mazao ya chakula.
Akiwa katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa huyo akamuagiza Mkurungezi wa Manispaa ya Singida kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa fidia kwa wamiliki wa makaburi yaliyopo soko la mahembe ili kupisha wafanyabiashara pamoja na kufanya marekebisho ya miundombinu katika baadhi ya maeneo hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge akizungumza wakati wa ziara hiyo
Aidha Dk. Mahenge kasisitiza ujenzi wa maegesho ya magari na sehemu za kushushia mizigo pamoja na kulifanya soko la Mahembe kama sehemu ya kushushia ndizi na viazi kutokana na maeneo mengine kuwa yameshajaa
Dk. Mahenge akaendelea kuitaka Manispaa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa ya kila kinachoendelea kuhusu fidia za makaburi na baadhi ya wamiliki wa nyumba ambazo zinatakiwa kupisha eneo la soko na kuwataka kuweka utaratibu ambao hautachelewesha utekelezaji wa shughuli hizo.
Naye Mkuu wa wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili akawataka wafanyabiashara hao kuhakikisha kwamba wanabaki katika maeneo yao waliyopangiwa wakati serikali ikiendelea kupambana na changamoto zinazojitokeza.
Mkuu wa wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili akizungumza wakati wa ziara hiyo
Aidha DC Muragili akawataka viongozi wa masoko kuelimishana ili kutoa ushirikiano wakati wa ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya masoko ikiwa ni pamoja na kukubali kufanya maendeleo wakati taratibu za malipo ya fidia yakiendelea.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Dk. Adrianus Kalekizi amemueleza Mkuu wa Mkoa kwamba Manispaa imejipanga kuhakikisha zoezi litakamilika ifikapo mwezi Mei 2022 ambapo kwa sasa tayari bajeti yake imeshapangwa.
Ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa iliwahusisha Viongozi wote wa Manispaa kamati ya ulinzi na usalama pamoja na wataalamu mbalimbali wa mazingira.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa Dk. Adrianus Kalekizi akielezea jambo wakati wa ziara hiyo
Baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Kilambida lililopo Singida Mjini wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo
Mwisho.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.