MKUU wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, ametoa siku saba (7) kwa halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Mkalama, Singida Dc na Manispaa kuhakikisha Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) inakamilika na kukabidhiwa ifikapo tarehe 25 Septemba mwaka huo.
Ametoa agizo hilo leo tarehe 18 Septemba, 2023 kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi alipokuwa akifanya ziara ya kukagua ujenzi wa miradi hiyo ambayo inasimamiwa na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri husika.
Serukamba akizungumza na Watendaji hao amesema kuwa Mkandarasi ambaye anachelewesha kazi wakati vifaa vyote vipo anatakiwa kupunguziwa kazi na kupewa mtu mwingine ambaye anaonesha kuwa na juhudi za kufanya kazi.
"Haiwezekani kuna vifaa vyote ambavyo vinastahili kutumika kwenye ujenzi lakini Mkandarasi anasuasua na napenda kuwaelekeza kama kuna hiyo hali Mkandarasi mpunguzie kazi na apewe fundi mwingine”
"Hatuwezi kuona kazi zinalala kwa ajili ya mtu ambaye anafanya makusudi au kama mtu mmepaana naye mfano milioni sita lakini kazi inaenda taratibu basi mwambie kuwa utampa milioni tatu na nusu na pesa nyingine atapewa mkandarasi ambaye ataweza kuendana na kasi inayotakiwa, nataka shule hizi nikabidhiwe tarehe 25 Septemba, 2023” Ameelekeza Serukamba.
Katika hatua nyingine amewaonya Wakandarasi ambao watachezea fedha za Serikali kwa kutekeleza miradi chini ya kiwango na kusema kuwa Wakandarasi hao hawatavumiliwa wala kufumbiwa macho na badala yake hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Aidha Serukamba amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo, hivyo hakuna atakaye kubali kuona fedha zinachezewa hivyo amesisitiza watendaji kuwa na nidhamu ya fedha na kutekeleza miradi ambayo itaonesha thamani ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya maendeleo na si vinginevyo.
Wakati huo huo Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri hizo pamoja na Wakandarasi wamesema kuwa watahakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kukabidhiwa tarehe 25 Septemba 2023 kama Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba alivyoagiza.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Singida ya kukagua miradi ya Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) itaendelea kesho tarehe 19 Septemba katika Wilaya ya Ikungi, Manyoni na halmashauri ya Wilaya Itigi wilayani Manyoni ikiwa ni kuhakiki miradi inayotekelezwa katika Mkoa huo inakamilika kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa.
SINGIDA
Anuani: P O BOX 5 SINGIDA
Simu: 2502170, 2502089
Simu: 2502170, 2502089
Barua Pepe: info@singida.go.tz ras@singida.go.tz
Copyright ©2023 Singida Regional Commisioner' Office . All rights reserved.